The House of Favourite Newspapers

TORONTO RAPTORS MABINGWA WAPYA NBA

TORONTO RAPTORS  kwa mara ya kwanza wamenyakua taji la ligi ya kikapu nchini Marekani NBA kwa ushindi wa michezo 4-2 dhidi ya mabingwa wa msimu uliopita Golden State Warriors.

Raptors wamemaliza kazi katika mchezo wa sita kwenye mfululizo wa mechi za fainali uliopigwa alfajiri ya leo kwa ushindi wa pointi 114-110 na hivyo kutokuwa na haja ya kumalizia mchezo wa saba ambao ungechezwa kuamua bingwa endapo Warriors wangeshinda.

Mchezo huo uliopigwa Oracle Arena nyumbani kwa Warriors ulikuwa mkali na usiotabirika kuanzia mwanzo hadi sekunde ya mwisho ukishuhudia Kyle Lowry akiibuka nyota wa mchezo kwa kuifungia Raptors pointi 26, assists 10 na rebound 7.

Katika hatua nyingine, mkali wa mabingwa hao wapya kutoka Canada, Kawhi Leonard, ameibuka mchezaji bora wa msimu (MVP), akiwa na wastani wa kufunga pointi 28.5, assists 4.2, na rebounds 9.8 katika kila mchezo kwenye hatua ya mtoano (playoff).

Walioipa ubingwa Raptors kwenye mchezo huo wa sita ni .

Kyle Lowry: 26 PTS, 10 AST, 7 REB
Pascal Siakam: 26 PTS, 10 REB
Fred VanVleet: 22 PTS, 5 3PM
Kawhi Leonard: 22 PTS
Serge Ibaka: 15 PTS .

Kabla ya ushindi huo, timu za Canada hazijawahi kuwa na cha kujivunia kwani mara zote huishia katika mashindano madogo. Taji la Raptors limemaliza nuksi ya timu za Canada kuendelea kuwa wasindikizaji, ambapo mara ya mwisho ilikuwa miaka 26 iliyopita (1993) pale Toronto Blue Jays iliposhinda taji ambalo hata hivyo si la NBA.

 

Katika ushindi huo, Nyota Kyle Lowry na Mcameroon Pascal Siakam wote wawili walifunga pointi 26 kila mmoja wakiongoza kwa pointi ikiwemo ribaundi 10 za Siakam na Asisti 10 pia za Lowry.

Upande wa Golden State Warriors, nyota Klay Thompson aliongoza kwa pointi zake 30 licha ya kushindwa kuendelea na mchezo dakika mbili za mwisho za robo ya kwanza katika kipindi cha pili akiumia mguu wa kushoto.

Kuumia kwa Klay ilikuwa pigo kubwa kwa Warriors kutokana na nyota huyo kutarajiwa kuamua mchezo wa leo baada ya kuwa na mchezo bora kabla ya kuumia baada ya nyota Steph Curry kudhibitiwa akifunga pointi 21 pekee.

 

Klay aliendeleza majanga kwa Warriors kufuatia kuumia kwake katika mchezo muhimu baada ya mchezo uliopita nyota mwingine Kevin Durant kuumia na kuipa pigo timu hiyo kujaribu kupindua matokeo ya 3-1.

Wachezaji wengine wa Warriors, Andre Iguodala alifunga pointi 22 wakati Draymond Green akitisha kwa kufunga pointi 11, ribaundi 18 na asisti 13.


Kwa matokeo hayo, Golden State Warriors wameshindwa kuendeleza ubabe waliokuwa nao ambapo walikuwa wametwaa taji hilo mara tatu ndani ya misimu minne iliyopita na walikuwa wanajaribu kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo.

KAWHI ABEBA TUZO YA MVP

Amevuna alichopanda!  Nyota Kawhi Leonard amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji mwenye thamani zaidi (MVP) wa mechi za fainali hiyo.

Katika mchezo wa mwisho leo alifunga pointi 22 pekee tofauti na mechi zilizopita na ribaundi sita na asisti tatu ikiwemo pointi zake za mwishoni zilizoihakikishia Raptors ushindi leo.

Tuzo hiyo ni ya pili kwake baada ya awali kutwaa mwaka 2014 akiwa na San Antonio Spurs ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwa timu hiyo akitokea kubadilishwa na DeMar DeRozan aliyeenda Spurs.

Comments are closed.