The House of Favourite Newspapers

Tox Star Afunguka Anavyomzimia Vee Money

TOX Star,MWANAMUZIKI anayefahamika zaidi kwa jina la TOX Star, alipotoa wimbo uitwao Pretty Girl, aliomshirikisha Ally Salehe Kiba ‘Alikiba’, ulimtambulisha vyema kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva.

Baada ya wimbo huo, kwa namna jamaa alivyowika kitaa na ngoma yake hiyo usingeweza kumtofautisha na majogoo waliokuwa wanawika mjini wakiwemo Alikiba mwenyewe.

Tox Star akawa Tox Star, tena akiwa chini ya Ostaz Juma na Musoma, baadaye akadondosha ngoma nyingine iitwayo Kitaani akimshirikisha Dully Sykes. Ngoma nyingine alizofanya zilikuwa ni pamoja na Karanga Mbichi aliyomshirikisha Lil Getto, Ole na Chukua, lakini hazikuweza kumrudisha kule alikokuwa kwenye ‘main stream.’

Pia kwa namna ambavyo hasikiki unaweza fikiri hayupo kwenye gemu tena. Risasi Mchanganyiko linakuletea huyu ili uweze kufahamu machache kutoka kwake kwa sasa. Ungana nami kwenye mahojiano naye.

Risasi: Hivi karibuni umerudi kwenye gemu na wimbo wa Chukua, mapokeo yake umeyaonaje na unafikiri wimbo huu utakurudisha kule ulipokuwa?

Tox Star: Ndiyo utanirudisha. Ninachokiona ni kwamba muziki wangu haujapoteza ‘vibe’ yoyote maana hata kwenye nafasi hii niliyopo wasanii wengi wanatamani kurudi lakini wanashindwa kufika.

Risasi: Lakini unahisi nini tatizo hasa mpaka ukapotea?

Tox Star: Kila kazi inachangamoto zake. Kwahiyo yapo mambo mengi ambayo yanapita yanaweza kumfanya mtu kurudi nyuma kimziki.

Risasi: Katika kazi zako zote bila shaka Pretty Girl ndiyo ilifanya vizuri zaidi?

Tox Star: Kazi zangu zote zimenipa mafanikio kwa sababu zimeongeza kitu kwa mashabiki wangu. Lakini tukizungumzia suala la kufanya vizuri ni kweli, na ninakumbuka sana nilivyokuwa ninasumbuliwa kwa shoo, ni tofauti na sasa.

Risasi: Ni kipindi gani ambacho huwezi kusahau kwenye game la muziki?

Tox Star: Mwaka juzi ulikuwa mzuri sana kwangu maana wimbo wangu niliofanya na Barnaba ulipata bahati kufika kwenye televisheni kubwa na za kimataifa ikiwemo Trace.

Risasi: Kuna wanamuziki wanaibuka na kuwapiga fimbo wakongwe, hili mnalizungumziaje?

Tox Star: Ni suala la kawaida kupeana nafasi. Kumbuka kila mtu anawakati wake wa kufanya vizuri. Ingawa hawa wa sasa hawawezi kuwa bora kuliko wakongwe.

Risasi: Kwa wanamuziki wa sasa, unamzimia mwanamuziki gani hasa kwenye suala zima la kufanya kazi.

Tox Star: Vee Money. Kiukweli huyo dada ninamzimia sana na siku moja nitafanya naye kazi. Nikibahatika mashabiki wangu watauona ule wimbo wa mwanamuziki kutoka Marekani, Nelly uitwao Dilema ukirudi tena kivingine.

Lakini niseme tu kwenye game la muziki Bongo miaka nenda rudi sijawahi kuona mtu wa kuzipa pengo la ‘role model’ wangu Albert Mangwea. Huyo siku zote ndiye mkali wangu.

Umewahi kuwaza kufanya kolabo na wanamuziki wa nje ili kujitangaza zaidi.

Tox Star: Ndiyo ni muhimu kuwaza hivyo. Nipo kwenye mipango mingi tu ya kazi na nimeshaanza mazungumzo na baadhi ya wanamuziki kadhaa, ni mapema sana kuwataja.

Risasi: Jambo la mwisho kwa mashabiki wako?

Tox Star: Ninawapenda na nitazidi kuwapa vitu vizuri, wasiache kunipa sapoti.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.