The House of Favourite Newspapers

Transparent Automobile: Magari Yanayoangaza Yaliyotengenezwa kwa Vioo Vitupu

0

 

MIEZI kadhaa iliyopita, katika maonesho ya magari ya Frankfurt Auto Show nchini Ujerumani, gari la kwanza la kisasa lililotengenezwa kwa vioo maalum viitwavyo Acrylic, lilioneshwa na kuwaacha wengi midomo wazi.

 

Kila kitu kimetengenezwa kwa kioo, isipokuwa matairi tu! Unaweza kuona kila kinachoendelea ndani ya mfumo wote wa gari, na mtu wa nje anaweza kumuona dereva kuanzia kwenye utosi wake mpaka kwenye unyayo!

 

Gari hilo limetengenezwa na Kampuni ya ZF ya nchini Ujerumani. Unaweza kudhani pengine teknolojia hii ni mpya lakini habari zikufikie kwamba gari la kwanza kabisa la vioo, lilitengenezwa mwaka 1939 na lilipewa jina la Pontiac Ghost na lilioneshwa kwa mara ya kwanza katika maonesho ya magari ya Futurama Exhibit jijini New York.

 

Ukiachana na toleo hilo la kale, toleo jipya lina mifumo mingi ya kisasa na hata mwonekano wake, ni wa kuvutia mno! Limefungwa vifaa vingi zikiwemo ‘sensors’, ‘airbags’ na kadhalika, kwa lengo la kuhakikisha kwamba dereva na abiria wake wanakuwa salama dhidi ya ajali za barabarani.

 

Kubwa zaidi, ni kwamba magari haya yamefungwa ‘rada’ maalum ambazo zitamsaidia dereva kugundua kwa haraka kama kuna ajali inakwenda kutokea mbele yake, ikiwemo kugongana na magari mengine au kuwagonga watembea kwa miguu na hivyo kumrahisishia dereva kuchukua hatua za haraka kuzuia ajali.

 

Pia magari hayo yamewekewa mikanda (seat belts) maalum ambayo itakuwa na uwezo mkubwa wa kumkinga abiria na dereva dhidi ya madhara yanayoweza kutokea wakati wa ajali, huku pia ikiwa imeunganishwa na ‘air bags’ ambazo hufyatuka wakati wa ajali na kuzuia madhara kwa watu waliomo ndani ya gari.

 

Lakini pia magari hayo yana teknolojia ya breki iitwayo IBCS, Integrated Brake Control System (IBC) ambayo inaliwezesha gari kufunga breki lenyewe kwenye mazingira hatarishi na hivyo kumpa nafasi zaidi dereva kufanya uamuzi sahihi wa kuepusha ajali.

 

John Plant, Mwenyekiti na Rais wa Kampuni ya TRW Automotive inayozalisha magari hayo, amenukuliwa akisema kwamba bado uboreshaji mkubwa unaendelea kufanyika na kuongeza teknolojia za kisasa kwenye magari hayo, ambayo ndiyo yanayotarajiwa kuwa chaguo la wengi kutokana na ubora wake, katika miongo kadhaa ijayo.

 

Ameongeza kwamba malengo yao ni kuiuza teknolojia hiyo kwa kampuni nyingine za utengenezaji magari zikiwemo Volkswagen (VW), Mercedes Benz, Ford, General Motors na Toyota.

 

Ni suala la muda tu kabla magari hayo hayajaanza kuonekana mitaani!

Leave A Reply