The House of Favourite Newspapers

Trump Atishia Kuuangamiza Uchumi Wa Uturuki

 

RAIS wa Marekani Donald Trump ametishia ‘kuiangamiza Uturuki kiuchumi’ iwapo taifa hilo litavishambulia vikosi vya Wakurdi nchini Syria baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka Syria.

 

Katika ujumbe  alioutuma kwenye mtandao wa kijamii  wa Twitter, Trump  amewataka pia Wakurdi wasiichokoze Uturuki.

 

Vikosi vya Marekani vimepambana kwa ushirikiano na wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mwa Syria dhidi ya kundi la Islamic State (IS).

 

Hata hivyo, Uturuki inawachukulia wapiganaji hao wa kundi la YPG kuwa ni magaidi.

 

Rais Recep Tayyip Erdogan ameshutumu vikali Marekani kuliunga mkono kundi hilo, na kuapa kuliangamiza.

 

 

Kauli ya Trump iliyotolewa jana (Jumapili) inafuata shutuma dhidi ya uamuzi wake wa ghafla wa kuondoa vikosi vya Marekani kutoka Syria.

 

Ofisa mkuu kutoka familia ya kifalme Saudia, Prince Turki al-Faisal, ameliambia shirika la habari la Uingereza (BBC) kwamba uamuzi huo utakuwa na ‘athari mbaya’ ambayo huenda upande wa  Iran, rais wa Syria Bashar al Assad na Urusi utafaidika kutokana nao.

 

Waziri wa mambo ya nje a Marekani, Mike Pompeo,  yuko Riyadh, katika mji mkuu wa Saudi Arabia, akizuru Mashariki ya Kati kuwahakikishia ushfirikiano washirika wa Marekani katika eneo.

 

Rais Trump ametetea uamuzi wake kuondoa vikosi hivyo, akieleza kuwa wapiganaji wowote waliosalia wa IS wanaweza kushambuliwa kutoka eneo ambalo halikutajwa, ‘lililopo katika kambi za karibu’.

 

Hakueleza namna uchumi wa Uturuki utakavyoathirika iwapo taifa hilo litawashambulia wapiganaji wa YPG.

 

Trump pia ametaja kuundwa kwa ‘eneo salama la maili 20’ ambalo mwandishi wa BBC, Barbara Plett Usher, amesema linadokeza aina ya suluhu ambayo Pompeo anajaribu kuijadili.

 

 

Rais pia alisema Urusi, Iran na Syria ndio wafaidi wakuu wa hatua ya Marekani Syria na kwamba wakati umefika kuwarudisha nyumbani wanajeshi wa Marekani.

 

Msemaji wa rais Erdogan Ibrahim Kalin amejibu katika ujumbe wa Twitter akisema Uturuki ilitarajia Marekani ‘kuheshimu ushirikiano wetu wa kimipango’.

 

“Magaidi hawawezi kuwa washirika na wandani wako,” alisema.

 

Trump aliwashangaza washirika na kukabiliwa na shutuma kali nyumbani mwezi uliopita walipoagiza vikosi vya Marekani kuondoka mara moja kutoka 30% ya maeneo yanayodhibitiwa na muungano wa vikosi Syria (SDF) unaoongozwa na YPG nchini Syria.

Comments are closed.