The House of Favourite Newspapers

Trump, Biden Wanyukana Tena Kwenye Mdahalo

0

WAGOMBEA wa urais wanaotajwa kuwa na nguvu zaidi nchini Marekani, Donald Trump wa Chama cha Republican na Joe Biden wa Chama cha Democratic, wamejitokeza katika vituo viwili tofauti vya televisheni katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na kituo cha Runinga ya ABC na NBC.

 

Katika mahojiano hayo kila mmoja alikuwa akimtupia lawama mwenzake, juu ya namna anavyouchukulia ugonjwa wa COVID-19, sambamba na siasa za ndani na za kimataifa.

 

Mahojiano hayo yamechukuliwa kama duru ya pili ya mdahalo wa ana kwa ana kati ya Trump na Biden, ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika jana, lakini Trump akajitoa baada ya waandaaji kuamua ufanyike kupitia mtandao.

 

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha ABC mjini Philadelphia, Biden alisema Trump hajayachukulia kwa umakini zaidi maradhi hayo, ambayo yashawaangamiza Wamarekani zaidi ya laki mbili.

 

Kwa mara ya kwanza Rais Trump amekubali kuachia madaraka kwa amani kama atashindwa uchaguzi wa mwezi ujao japo ameonyesha wasiwasi wake kuhusu ulinzi wa kura,  hata hivyo, wasimamizi wa uchaguzi huo wamesema kuwa hakuna ushahidi wowote unaoonyeshwa kusambazwa kwa karatasi za kupigia kura kabla ya uchaguzi.

 

Katika mahojiano hayo yalioendeshwa na kituo cha NBC kilichopo Miami Florida, Trump aliulizwa kuhusu nadharia ya kishetani inayojihusisha na biashara ya watoto wadogo (QAnon) ambapo alijibu kwa kuikataa nadharia hiyo na kusema kuwa haitambui.

 

Biden aliulizwa iwapo anaunga mkono kuongezwa kwa wajumbe wa mahakama kuu kwa lengo la kushawishi usawa wa kiitikadi ambapo alisema kuwa ataangalia namna ya kuifanya mahakama ifanye kazi kama mhimili wa pili wa serikali na hajawahi kuamini katika kubana uhuru wa mahakama.

 

Mdahalo mwingine wa wagombea hao utafanyika Oktoba 22, mwaka huu katika utaratibu ambao bado haujafahamika.

 

Leave A Reply