The House of Favourite Newspapers

Tukinawa Mikono Kwa Chid Benz, Nani wa Kutulaumu?

0
Chid Benz akitiwa mbaroni.

CHID Benz tena. Mwanzo alikataa sana, akafikia kipindi akawa hadi anatukana kila alipoulizwa kuhusu kubwia unga, lakini baada ya matumizi yake kumdhibiti, mwenyewe akalazimika kunyoosha mikono na kuomba msaada.

Walijitokeza watu kumsaidia, tena wakitumia muda wao na fedha zao, lakini kama anayecheza filamu za kitoto, akawatoroka na kurejea tena mtaani akiishi kama chokoraa, wale watoto wasio na walezi, wanaozurura wakiiba na kidogo wanachopata, wananywea pombe na kubwia unga.

Kwa mtu ambaye unasoma tu magazeti na kutazama picha zake, huwezi kunielewa ninachokizungumza. Ninamzungumzia Chid Benz, ambaye alishafikia kiwango cha kuvaa ndala zenye rangi tofauti, tena akiwa mchafu kama wale wapiga debe mateja, unaowaona kwenye vituo vya daladala.

Unamzungumzia staa ambaye kwenye ‘dashbodi’ ya gari yake kulikuwa kunakaa milioni kadhaa, lakini hadi akafikia kiasi cha ‘kupiga mzinga’ shilingi mia mbili, achangechange akanunue japo kete moja ya cocaine avute, apate stimu!

Bado, watu wenye uchungu naye wakakataa kushindwa, wakamtoa katika hali hiyo na

kumrejesha tena kwenye vituo vya kurekebisha watu walioathirika na madawa ya kulevya, ili asaidiwe. Na huko kote, ni fedha zinatumika, kwanza za kumliwaza yeye mwenyewe, lakini pia za kugharamia matibabu yake.

Alipotoka sober house mara ya mwisho, akitokea Mafinga mkoani Iringa, miezi michache iliyopita, huyu jamaa wa Ilala, aliahidi kuwa sasa ameachana kabisa na madawa, kwamba ni mtu mpya na aliweza hata kufanya ngoma moja na Q Chillah iitwayo Muda.

Wengi walimkubali na kuamini kuwa amerejea kuwa yule King Kong tunayemjua. Lakini kumbe Chid bado hana hata nia ya kuachana na ubwiaji unga.

Ni hapa ndipo ninapojaribu kuwaza kwa sauti. Hivi inawezekanaje watu wakaelekeza mapenzi yao ya dhati kabisa kwa mtu ambaye hajipendi? Yes, Chid Benzino hajipendi, anataka kujimaliza, lakini watu wanamlazimisha abaki, kwa nini?

Chid Benz.

 Kuna mamia ya vijana waathirika wa madawa ya kulevya Tanzania nzima ambao wanatamani atokee mtu mwenye roho kama za wale wanaomsaidia Chid, ili nao wapate tiba warejee katika maisha yao ya kawaida. Nenda pale Mwananyamala Hospitali, kitengo kile cha kutoa dawa za kuwasaidia wabwia unga uone jinsi vijana wanavyohangaika.

Badala watu kukomaa na mtu ambaye hajipendi, hajijali na wala hana mpango wa kujionea huruma, ni bora wasamaria wema hawa, wakawaokoa vijana waliojaa huku mitaani, ambao baadhi yao walijiingiza katika matumizi ya madawa haya kwa kuwaiga akina Chid Benz na sasa wanashindwa namna ya kujiokoa.

Na kusema ule ukweli, nimeamua kumuelewa Chid Benz na kuuheshimu uamuzi wake. Hata kama hatuwezi kumhukumu kwamba kakutwa na unga, lakini kuwemo katika kundi lenye watu wa aina hiyo, ni wazi kuwa bado anatembea katika mazingira yaleyale.

Ameamua kusimamia kile anachokiamini kuwa kwake yeye, kubwia unga ni jambo muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote na nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa anafanya haya kwa bahati mbaya au eti arosto imemzidi.

Anajua anachokifanya na huenda anatushangaa mno tunavyompigia kelele kwenye starehe zake, kama ambavyo hata mimi huwa sipendi watu wanapoanza kunisimanga kwa starehe zangu.

Kama nafasi hii ndogo iliyobaki ataruhusu imponyoke katika kujiokoa na matumizi ya madawa, kama dalili zote zinavyoonyesha, ni suala la muda tu kumuona tena yule mkali wa Rap, aliyekuwa na mwili mkakamavu, akirejea tena katika mitaa ya Kinondoni, akiwa mchafu na ombaomba.

Ule msemo wa bahati haiji mara mbili haijawahi kufanya kazi kwa King Kong, kwa sababu hii ni zaidi ya mara ya tatu watu wanajitokeza kumsaidia lakini anaichezea!

 

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Shamrashamra Mapokezi ya Watoto wa Shule ya Lucky Vincent KIA

Leave A Reply