The House of Favourite Newspapers

Tukio la Scorpion Lajirudia Dar, Mwingine Atobolewa Macho, Tumbo

kipofu-tukio-la-scorpioni-1 Rashid Mohammed akieleza alivyotobolewa macho.


Stori: Issa Mnally, Gazeti la Risasi Jumamosi, Toleo la Desemba 31, 2016

DAR ES SALAAM: Hii ni ajabu na kweli! Wahenga walisema hakuna kumbukumbu isiyokuwa na mwenzake, ni kweli kabisa! Lakini msemo huo umenogeshwa zaidi na tukio la kijana mjasiriamali aliyejulikana kwa jina la Rashid Mohammed (28) kutobolewa macho na kupasuliwa tumboni kwa visu na vibaka na hivyo kuumaliza mwaka kwa kutoona, inauma sana!

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni maeneo ya Kigogo jijini hapa ambapo Rashid alikuwa kwenye bodaboda akitokea kwenye ukumbi wa starahe wa Ambiance, Sinza Afrika Sana kurudi nyumbani kwake, Kigogo.

said-mrisho-pics-02

Said Mrisho anayedaiwa kutobolewa macho na scorpion.

TUKIO KAMA HILO

Tukio la Rashid kutobolewa macho na kumsababishia upofu sanjari na kujeruhiwa tumboni linafanana kwa asilimia 95 na tukio lilimtokea mjasiriamali Said Mrisho (32), ambaye Septemba, mwaka huu maeneo ya Buguruni Kwamnyamani alivamiwa, akaporwa vitu, akajeruhiwa tumboni na kutobolewa macho na mpaka sasa haoni.

Katika sakata la Said, mcheza kareti, Salum Njwete ‘Scorpion’ ndiye aliyedaiwa kuhusika baada ya kutajwa na kesi yake iko Mahakama ya Ilala, Dar ikiendelea kusikilizwa. Jina la Scorpion likaondokea kuwa maarufu sana miongoni kwa jamii kutokana na kesi yake kuteka hisia zao. Sehemu kubwa ya Watanzania, wanajua Scorpion ni nini!!

kipofu-tukio-la-scorpioni-4SIKU YA TUKIO LA RASHID

Kwa mujibu wa Rashid mwenyewe, siku ya tukio la kutobolewa macho ilikuwa saa tisa usiku, alikuwa akitoka klabu kufurahia maisha baada ya kazi ngumu za mchana kutwa, lakini alipofika kwenye eneo linaloitwa Darajani akiwa amepanda pikipiki, ghafla walitokea vibaka na kusimama katikati ili kuwavamia.

Alisema: “Kuona vile, dereva aligeuza bodaboda ili turudi tulikotoka, lakini bahati mbaya mimi nikaanguka. Ndipo wale vibaka wakaja kunivamia, wakanichoma visu tumboni, machoni na shingoni kisha wakanimwagia mchanga machoni wakati damu zinatoka.”

kipofu-tukio-la-scorpioni-2

AMULIKWA NA TOCHI ASIWATAMBUE

“Lakini kabla ya kunifanyia vile, walinimulika kwanza na tochi. Nadhani lengo lao lilikuwa ni kunifanya nisiwatambue, maana mwanga wa tochi uliponiingia machoni hakuna niliyemtambua.”

APOTEZA FAHAMU, AZINDUKIA MWANANYAMALA

“Nililala chini nikiwa nagalagala na maumivu makali sana mpaka nikapoteza fahamu. Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nipo Hospitali ya Mwananyamala, lakini hali yangu ilipozidi kuwa mbaya nilikimbizwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.”

VITU ALIVYOKOMBWA

Anaendelea: “Wale vibaka walifanikiwa kunipora simu ya mkononi yenye thamani ya shilingi laki tatu na elfu thelathini (330,000), shilingi elfu arobaini na tano taslimu (45,000) zilizokuwa kwenye waleti na viatu nilivyovaa siku hiyo.”

BAADA YA HAPO?

“Wale watu walikamatwa na vijana wa mtaani ambao walisema wanawafahamu. Walifanya msako wakawashika na kuwafikisha kwenye Kituo cha Polisi Magomeni ambako walikuja kuachiwa baadaye.”

AWAOMBA MADAKTARI WAMCHOME SINDANO YA SUMU

“Nikiwa Muhimbili kwa kweli maumivu yalikuwa makali sana. Lakini pia niliumia sana baada ya daktari aliyenifanyia upasuaji kusema kwamba, kwa jinsi macho yangu yalivyotobolewa, siwezi kuona tena!

“Awali nilihisi kama nimesikia vibaya lakini nilipohakikisha kwamba nilichoambiwa ndicho kwamba sitaona tena, nikahisi daktari alitaka kufanya utani na mimi kabla ya kuniambia ukweli, lakini msisitizo wake ukawa hivyohivyo, kwamba mimi Rashid siwezi kuona tena.

“Nililia sana, nikamwomba daktari kama kuna uwezekano anichome sindano yenye sumu ili nife kuliko kuanza kuishi maisha ya kutoona lakini daktari akaniambia hakuna kitu kama hicho na kujaribu kunitia moyo na kunijengea matumaini.

“Unajua kwa mtu ambaye ulikuwa unaona kama wengine na kufanya shughuli zako za kila siku halafu itokee ukawa huoni, tena kisa amekisababisha mwanadamu mwenzako kwa makusudi, inaumiza sana kwa kweli.”

ATOKA HOSPITALI AKIWA HAONI!!

“Baada ya kutibiwa pale Muhimbili kwa siku kadhaa, niliruhusiwa kutoka lakini tayari nilikuwa sioni. Nilisaidiwa na ndugu kufika nyumbani kwa kuelekezwa kwa kupita mpaka kwenye gari na kwenda kushuka kuingia ndani nyumbani.”

scorpioni-1

Scorpion akipelekwa mahakamani.

UWIANO WA RASHID NA SAID

Wakati Rashid alikumbwa na dhahama hiyo akiwa kwenye usafiri wa bodaboda kurudi kwake, Said yeye alitoka kushuka kwenye usafiri wa Bajaj akinunua kitowea naye akirudi kwake.

Wakati Rashid alikombwa shilingi 45,000, viatu na simu ya mkononi, Said yeye alikombwa shilingi 300,000, simu ya mkononi na mkufu wa silva.

Wakati Rashid alikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala kisha Muhimbili, Said alikimbizwa Hospitali ya Amana, baadaye Muhimbili. Wote waliambiwa na madaktari kwamba hawataona tena. Sehemu alizojeruhiwa Rashid, tumboni na machoni ndizo hizohizo alizojeruhiwa, Said.

RASHID ALIKUWA NA MKE

“Mimi kabla ya kupata hiki kilema nilikuwa na mke na tulikuwa tukiishi vizuri tu. Lakini baada ya kupata huu ulemavu, mke wangu aliondoka. Yeye anajua sababu, lakini aliondoka.”

Tofauti, mke wa Rashid aliondoka, mke wa Said anakomaa na mumewe mpaka sasa.

risasi-1

Gazeti la Risasi Jumamosi, Toleo la Desemba 31, 2016

ALICHOJIFUNZA RASHID

“Mimi nakubaliana na methali ya wahenga kwamba, Hujafa Hujaumbika. Walikuwa na maana kwamba, mtu siku ukifa, vile unapelekwa kuzikwa kaburini ndiyo ukamilifu wa kuumbwa kwako. Ukifa huna mkono, ndiyo utakuwa huna mkono hadi kaburini, ndiyo ukamilifu wa kuumbwa kwako.

“Neno hujafa linaamanisha kama mimi hivi, nilikuwa naona lakini kabla sijafa nimekuwa sioni. Kwa hiyo kumbe siku zote nilikuwa sijaumbika. Na pia si kama nimeshaumbika, maana sijui ya kesho. Siku nikifa nikiwa hivi ina maana ndiyo nitakuwa nimeumbika, yaani vile nitakavyokuwa naingia kaburini.”

KIKUBWA KWA RASHID

“Mimi kwa sasa naishi kwa kuombaomba, nasaidiwa tu na washikaji zangu na Mungu awabariki sana. Lakini nahisi kama nawapa mzigo mkubwa. Ningeomba kwa mtu yeyote ambaye ataguswa na hili tukio langu anisaidie kwa njia yoyote ile niweze kupata kitu kitakachonifanya niendeleze maisha yangu katika hali hii.

 

“Pia kama mtu ana chochote anataka kunitumia ili niweze kujikimu kwa chakula anaweza kunitumia kwa namba 0713 340660.

 

Tukio la Scorpion Lajirudia, Bodaboda Atobolewa Macho (Part 01)

Tukio la Scorpion Lajirudia Dar, Bodaboda Atobolewa Macho (Part 02)

Comments are closed.