The House of Favourite Newspapers

TUNACHOJIFUNZA MAUAJI YA KIMBARI RWANDA-4

ILIPISHIA WIKI ILIYOPITA…

Watanzania wengi hawajui nini kilisababisha mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa kikatili. Naamini kama wakisoma makala haya watajifunza kitu na kuona umuhimu wa mshikamano na amani tulionao na faida yake. SASA ENDELEA…

 

UMEKWISHAONA kuhusu jumba la makumbusho lililopo jijini Kigali, Rwanda lililobeba historia ya kutisha ya mauaji ya kinyama ya kimbari. Kwa nje ya makumbusho hayo kuna makaburi makubwa walimozikwa mamia ya watu. Lipo kaburi la wazi la kioo.

Inaelezwa kwamba, baada ya machafuko ya vita ikawa mamia ya mafuvu ya binadamu yaligunduliwa sehemu mbalimbali hivyo kuchukuliwa na kuja kuzikwa mahali hapo kiheshima.

 

Wiki ijayo tutaangalia historia ya Rwanda kabla ya mauaji haya au kabla ya ukoloni, lakini leo tutazungumzia maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji hayo ya kimbari ya Rwanda yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, Jumamosi iliyopita, Aprili 7, mwaka huu na gazeti hili kualikwa.

Mengi yalisemwa katika hafla hiyo ambayo ilikuwa siyo ya kufurahisha kutokana na maneno yaliyokuwa yakizungumzwa.

 

Kuna ushuhuda wa waliopata madhara na mauaji hayo ulitolewa na mwanamke mmoja kupitia video. Maneno ya mama huyo yaliwafanya baadhi ya waliohudhuria kububujikwa na machozi.

Alieleza alivyopoteza ndugu zake, mumewe na watoto huku yeye akiponea chupuchupu kufariki dunia mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbari Rwanda kutokana na jinsi alivyobakwa na baadaye kupigwa kulazimishwa kunywa damu za maiti kisha kukatwakatwa na watu aliowaita Interahamwe.

 

Mama huyo alisema baada ya kukatwakatwa, wauaji waliamini kwamba ameshafariki dunia, hivyo alikusanywa na maiti na kwenda kutupwa kwenye shimo moja refu sana.

“Nikiwa ndani ya shimo nilipata fahamu Mungu akanisaidia nikapata nguvu ya kuita watu ili waje kuniokoa.

 

“Bahati nzuri Mungu alinisikia akaja mtu mmoja na kuniuliza kama nimeumia sana au ninaweza kusimama, alisema kama nitashindwa kutembea hataweza kuniokoa.

“Hata hivyo, mtu huyo alisema nisipige kelele kwa sababu wauaji wa Interahamwe bado wapo na wanaweza kuja kunimaliza, akaniomba nisubiri kwa moyo wa imani kwani atarudi kunitoa humo shimoni.

 

“Baada ya muda, mtu yule alikuja na kuniuliza kama naweza kusimama, nikamwambia siwezi, akasema je, nitaweza kujifunga kamba? Nilimwambia siwezi kwa kuwa mkono wangu umekatwa.

“Mtu yule akasema kama ni hivyo hataweza kuniokoa, hata hivyo, alinirushia kamba akaniambia nijifunge kifuani vizuri ili nivute na kunitoa nje ya shimo hilo refu.

“Niliiona ile kamba ingawa mkono wangu ulikuwa umekatwa nilijitahidi na Mungu alinisaidia nikajifunga ile kamba kifuani kama alivyoelekeza yule mtu na akaanza kunivuta taratibu mpaka akanitoa nje ya lile shimo.

“Baadaye alinipeleka kanisani, niliangalia mguu wangu wa kulia na kukuta una tundu kubwa, sijui walinifanya nini baadaye walinikimbiza katika Hospitali ya King Faisal ambapo nilipewa matibabu.

“Nilitibiwa na kupona, lakini nimebaki kuwa kilema, siwezi kufanya kazi yoyote, sina nyumba, sina ndugu na sina lolote la kuniingizia kipato,” alisema mama huyo na kuacha simanzi ukumbini ambapo kulikuwa na baadhi ya mabalozi kutoka nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchini.

 

Baadaye Balozi wa Rwanda nchini, Eugene Kayihura alisimama na kusema nchini Rwanda mauaji ya kimbari watu wanadhani ni ya kikabila, lakini ukweli ni kwamba yalilenga watu fulani.

Aliwaomba watu wote, siyo Rwanda tu, bali dunia nzima kutoruhusu mauaji kama hayo kutokea. Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema mauaji hayo yalifanya Wanyarwanda wengi kukimbilia Tanzania.

 

“Mwaka 2016, rais wetu, Dk John Magufuli alitembelea Rwanda pale Kituo cha Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari Rwanda mjini Kigali akasema mauaji haya yasitokee tena, siyo Rwanda ila sehemu yoyote Tanzania.

Akaongeza kuwa, alisema hatuwezi kubadilisha kile kilichotokea, lakini akasema mauaji ya kimbari hayaji kama radi, bali ni kwa kupandikiza chuki katika jamii, jambo ambalo tunapaswa kulipinga watu wote katika dunia hii.

Nini kilifuata? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Comments are closed.