The House of Favourite Newspapers

Tusiruhusu amani ivurugwe nchini

0

amaniTUPO kwenye kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, tumuombe Mungu siku hiyo ikifika tupige kura kwa amani na kupata viongozi wetu kwa njia ya haki.

Nianze kwa kusema kila mtu mzalendo wa nchi hii anaombea uchaguzi huo uwe wa haki na amani itawale kwa sababu baada ya kupiga kura, kuna maisha yatakayoendelea kwa kila Mtanzania na hata kwa raia wa nje aliyeko nchini.

Kabla ya kampeni kulikuwa na makongamano ambapo hata Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kiliwahi kuandaa kongamano la siku mbili lililokuwa na lengo la kutafakari amani ya taifa ambalo liliwashirikisha viongozi mbalimbali waandamizi wa vyama vya siasa na serikali wakiwemo mawaziri.

Kongamano hilo lilikuwa zuri na nimelikumbuka kwa sababu hivi sasa kuna viashiria vingi vya uvunjivu wa amani nchini.

Kumekuwepo kiwango kidogo cha uvumilivu wa kisiasa na dini miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa na dini na kumekuwa na waandishi wa habari wanaopuuza maadili na kuandika na kutangaza habari za uongo, uchochezi na uchonganishi ambao unafanywa pia na mitandao ya kijamii. Unayefanya hivyo unajua kwamba unataka kuingiza nchi katika janga zito?

Tanzania imepata fursa ya kuwa kisiwa cha amani kiasi cha kutolewa mifano duniani hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuienzi na kuilinda kwani historia inaonesha nchi nyingi zilizopoteza amani hadi sasa zinaishi kwenye machafuko.

Amani ni tunu ambayo nchi nyingi zinaililia, sisi tumebahatika kuwa nayo tusiichezee wala kuwaruhusu watu wengine waichezee, ikishatoweka huwa hairudi.

Nawahimiza Watanzania kuendelea kupendana, kwani nchi ambazo amani imetoweka zimekuwa na vilio kila kukicha na uchumi wao kudidimia kwa kuwa wanakosa muda wa kushiriki shughuli za kuzalisha mali.

Amani tuiimarishe kwani nchi inapokosa amani wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto, ambao wanakosa huduma muhimu kama maji, dawa na wanawake ni wadau wakubwa wa amani na wanatakiwa wakishawagundua viongozi wenye viashiria vya uvunjivu wa amani wawaadhibu kwa kuwanyima kura.

Vyama vya siasa vinatakiwa kuwa na mfumo wa kuwashirikisha wanawake kulinda na kudumisha amani ya taifa, mchango wa wanawake katika malezi ya familia, uongozi na uzalishaji mali ni mkubwa sana una umuhimu wa kipekee katika kudumisha amani na kuleta maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ni jukumu la wanasiasa kujenga amani na siyo kuchonganisha kwenye maeneo yote ya nchi na kwamba badala ya kukaa mijini tu waende hata vijijini, katika kata wawakutanishe viongozi wao na kuwapa elimu juu ya amani wakati huu wa kampeni za uchaguzi kabla mambo hayajaharibika.

Nashauri hivyo kwa sababu kuna viashiria vya dhahiri vya uvunjifu wa amani kwa kuwa kuna watu wamekuwa wakiwapiga wenzao, kuwaumiza na kuwaua kwenye mikutano ya kampeni hivyo nahimiza zifanyike  jitihada za haraka kukomesha tabia hiyo.

Hakika hali kwa sasa siyo shwari kwa upande wa amani ya nchi na ni jukumu la kila mmoja kuhimiza amani kwa kuwa ikitoweka hata serikali itashindwa kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi ambao nao watashindwa kufanya shughuli zao mbalimbali.

Wanasiasa waache kutumia lugha za matusi na kudhalilisha mamlaka zilizopo madarakani au kukashifiana wao kwa wao kwani kufanya hivyo kunawafanya wafuasi wao kuchukiana. Nchi  hii ina historia tukufu tangu enzi ya       uongozi wa  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia mbinu za ulaghai, vitisho, uzushi, uongo, rushwa, kebehi na matusi kama mtaji wao kisiasa kwenye kampeni zao, jamani nawaomba waache kufanya hivyo, kampeni ziwe za kistaarabu. Tusiruhusu amani ya nchi ivurugike.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply