The House of Favourite Newspapers

Tuwape Moyo Serengeti Boys Wafanye Maajabu Afcon

MICHUANO ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Vijana chini ya umri wa 17, ipo karibu kuanza. Itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Aprili 14 hadi 28, mwaka huu.

 

Tanzania ndiyo wenyeji na Serengeti Boys ambayo kwa sasa ipo nchini Uturuki ikishiriki mashindano ya Uefa Assist, ndiyo itatuwakilisha. Kupitia mashindano hayo ambayo Serengeti Boys imecheza mechi mbili tayari, ikifungwa na Guinea na kushinda dhidi ya Australia, itatusaidia katika kuijenga timu hiyo.

 

Kucheza na timu zilizokuwa juu yako kwenye viwango vya soka duniani ni sehemu ya kujifunza kutokana na makosa ambayo huwa mnafanya kila siku. Tazama Serengeti Boys ilivyofungwa na Guinea, wapo waliobeza na wengine waliipa moyo timu hiyo, mechi iliyofuata ikashinda, sasa watu wote wameungana kuipongeza. Katika mashindano kama haya ambayo ni sehemu ya maandalizi ya mashindano makubwa, timu kupoteza ndiyo huwa inajifunza zaidi kuliko ikiwa inashinda tu.

Kama mtakuwa mnakumbuka, Serengeti Boys ile ambayo ilienda kushiriki Afcon nchini Gabon mwaka 2017, katika mechi zake za kufuzu na zile za kirafiki ilifanya vizuri sana, tukaamini kwamba tuna timu imara ambayo itatusua kwenye michuano hiyo. Kilichotokea ni kushika nafasi ya tatu kwenye kundi na kushindwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo.

Tunatakiwa kujifunza kutokana na hilo, tunapoona hivi sasa vijana wetu wanapoteza mechi katika kipindi hiki cha maandalizi tunatakiwa tuelewe kwamba wapo katika kujiweka sawa. Benchi la ufundi linapoona limepoteza mechi, kuna vitu wanavibaini kwamba wapi wamekosea, hapo inakuwa rahisi kwao kurekebisha kuona timu inakuwa imara zaidi pindi mashindano yatakapoanza.

 

Tukianza kuibeza Serengeti Boys hivi sasa katika mashindano ya Uefa Assist, hatutakuwa tunajenga kitu, bali tutakuwa tunabomoa na mwisho wa siku tutatia aibu hapa nyumbani

Comments are closed.