The House of Favourite Newspapers

Tuzo Ya Kiswahili Ya Safal-Cornell Ya Fasihi Ya Afrika: 2021 Yatoa Orodha Ya Miswada

0
Meneja Uhusiano wa Alaf Ltd Hawa Bayuni (kulia) akizungumza kwenye mkutano na wanahabari kushoto ni Afisa Uhusiano wa Alaf Ltd Theresia Mmary.

Januari 10, 2023, Nairobi…… Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika imetangaza orodha fupi ya miswada ya mashindano ya mwaka 2022.

Tuzo hii inafadhiliwa na kampuni ya Safal Group, kupitia matawi yake ya Mabati Rolling Mills, Kenya; na ALAF, Tanzania; Kituo cha Taaluma za Afrika katika Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani; na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, baina ya lugha hizo na kwa lugha hizo.

Mwenyekiti wa majaji wa mwaka huu, Profesa F.E.M.K. Senkoro, alipotoa uamuzi wao alisema kwamba kupokelewa kwa idadi kubwa sana ya miswada ya riwaya na ushairi, kutoka sehemu mbalimbali za Afrika, hasa Afrika ya Mashariki, ni dalili tosha kuwa tunayo hazina kubwa ya ubunifu, hasa miongoni mwa vijana, ivukayo mipaka ya nchi mojamoja, na ambayo ikimwagiliwa maji ya misingi ya uandishi na uchapishaji wa kazi za kifasihi itaiimarisha sana tasnia ya fasihi ya Kiswahili.

Hawa Bayuni akisisitiza jambo.

“Miswada mingi iliyoshindanishwa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika ya Mwaka 2022, ilikuwa mizuri sana hadi kuifanya kazi ya majaji kuwa ngumu mno katika kuamua kazi zipi zipewe ushindi.

Kwa hakika, karibu miswada yote iliyopitiwa na majaji ilistahili ushindi wa namna moja ama nyingine, lakini kwa vile kwenye ushindani wa aina hii hapana budi apatikane mshindi, basi kwa kauli moja majaji walipitisha maamuzi magumu ya majina ya washindi yatakayotangazwa.

Maamuzi yalizingatia umahiri, ustadi, na hata upya/upekee, wa kuoanisha vipengele muhimu vya kifani na kimaudhui kulingana na utanzu husika.” alisema Profesa F.E.M.K. Senkoro wakati wa tangazo hilo.

Waliojiunga na Profesa F.E.M.K. Senkoro katika kusoma na kuiteua miswada ya mashindano ya mwaka 2022 walikuwa ni Dkt Magdaline Nakhumicha Wafula wa Chuo Kikuu cha Moi, na Dkt Hamisi Babusa wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya.

Majina ya waandishi na miswada iliyoingia katika Orodha Fupi ni kama ifuatavyo. Katika utanzu wa Riwaya miswada iliyoteuliwa ni Dunia na Watu Wake – Ahmad Simba Mwaita (Tanzania), Wimbo wa Hatima – Isaac Ndolo (Kenya) na Ujanajike – Dotto Daudi Rangimoto (Tanzania).

Katika utanzu wa Ushairi miswada iliyoteuliwa ni Mzoga Unaonukia – Lenard Mtesigwa (Tanzania), Mamangu Nipe Wosia – Salum Makamba (Tanzania) na Uswahilini – Ally Bakari Mchanyato (Tanzania).

Washindi watakaotokana na orodha hii fupi watatangazwa katika sherehe itakayofanyika tarehe 25 Januari, 2023, jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Vigezo vya Tuzo ya Kiswahili:

Zawadi zinatolewa kwa miswada bora zaidi ambayo haijachapishwa katika tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za michoro. Zawadi za jumla ya dola za Marekani 15,000 zitagawanywa kama ifuatavyo:

Zawadi ya kwanza ya Riwaya – Dola 5,000

Zawadi ya kwanza ya Ushairi – Dola 5,000

Zawadi ya pili katika utanzu wowote – Dola 2,500

Mbali na zawadi hizo, miswada iliyoshinda itachapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, Tanzania. Na miswada ya mashairi itakayoshinda itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.

Kwa Wahariri:

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za michoro. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota Publishers. Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation).

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini.

ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

Ngugi Wa Thiong’o Foundation Wakfu huu unapata nguvu zake kutokana na hamu na ari ya kukuza kuonekana kwa Lugha za Kiafrika nchini Kenya, barani Afrika, na duniani, na kutambuliwa kuwa ni vyombo mwafaka vya kuendeshea shughuli za sanaa ya uigizaji, ubunifu, uvumbuzi, na taaluma. Pia unazitambua lugha hizi kwamba zina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kila fani – tangu utamaduni, sayansi za kibiolojia, teknolojia hadi tiba. http://ngugiwathiongofoundation.org

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.”

Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 likaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma Wa Ngugi, Lizzy Attree, Walter Bgoya, Sarit Shah, Anthony Ng’ang’a, Henry Chakava, Chege Githiora, Clarissa Vierke, Farouk Topan, Carole Boyce Davies, and Ngugi Wa Thiong’o.

Mkurugenzi: Munyao Kilolo

Majaji: Prof. F.E.M.K. Senkoro ana shahada za B.A. (Education), M.A (Kiswahili) na Ph.D. (Kiswahili) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na M.A. (Fasihi Linganishi) kutoka Chuo Kikuu cha Alberta, Canada.

Pamoja na kufundisha Kiswahili kwa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kabla ya kustaafu Profesa Senkoro alikuwa pia Mratibu wa Kituo cha Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi za Kiafrika na Mkuu wa Idara ya Fasihi zote katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI); na Mkuu wa Kitivo Mshiriki (Utafiti na Machapisho) katika kilichokuwa Kitivo cha Fani na Sayansi za Jamii katika chuo hichohicho.

Wakati huohuo, kwa mihula miwili mfululizo, Profesa Senkoro alikuwa katika Kamati ya Utendaji ya Baraza la Maendeleo ya Utafiti wa Sayansi za Kijamii Afrika (CODESRIA) kama Mwenyekiti wa Kamati

Ndogo ya Utawala Bora. Vilevile Profesa Senkoro amekuwa Mwanazuoni na Profesa Mualikwa katika vyuo vikuu mbalimbali vikiwemo vya UNISA na Durban-Westville, Afrika Kusini; Wisconsin-Madison, Boston, Harvard, na Princeton nchini Marekani; na Chuo Kikuu cha Namibia (UNAM).

Amechapisha zaidi ya makala 100 zihusuzo vipengele mbalimbali vya fasihi ya Kiafrika, hasa ile ya Kiswahili, na pia vitabu 12 vikiwemo vya nadharia ya fasihi, riwaya mbili na diwani moja ya hadithi fupi. Amepata tuzo kadhaa ikiwemo ya CODESRIA kwa ajili ya uandishi wa kazi yake ya “The Social Significance of the Journey in Folktales from Zanzibar”;

Tuzo ya Rockefeller African Humanities Institute, W.E.B. Du Bois Institute for Afro American Research, ya Chuo Kikuu cha Harvard (2000 –2001); na Nishani ya Kiswahili ya Shaaban Robert iliyotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) (2001).

Kwa sasa, zaidi ya kufundisha kozi za uzamivu za fasihi ya Kiswahili katika vyuo vikuu kadhaa, Profesa Senkoro anaendelea na uandishi wa vitabu na makala mbalimbali kuhusu lugha, fasihi na utamaduni wa Kiswahili.

Dkt. Magdaline Nakhumicha Wafula ana shahada za B.A. (Honours) na P.G.D.E. kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, MPhil (Kiswahili) kutoka Chuo Kikuu cha Moi na Ph.D. (Fasihi za Kiafrika) kutoka Chuo Kikuu cha Bayreuth, Germany. Amekuwa akifundisha lugha na fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi,Eldoret tangu mwaka 2014.

Kwa sasa anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika. Amefanya utafiti katika vitengo vya Isimujamii, riwaya ya Kiswahili, Tafsiri na masuala ya Jinsia. Anachangamkia zaidi tanzu za kinathari na hasa riwaya ya Kiswahili.

Tasnifu yake ya Uzamifu ni tahakiki ya migogoro ya vizazi katika riwaya za Vuta n’kuvute,Kufa Kuzikana, Kipimo cha Mizani na Tumaini. Ameandika na kuchapisha tahakiki juu ya Kisima cha Giningi, Msimu wa Vipepeo, Nakuruto, Unaitwa Nani?Dunia Yao, Babu Alipofufuka na Bin-Adamu!

Pamoja na kufundisha kozi za fasihi ya Kiswahili kwa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Moi, amesimamia na kutahini zaidi ya tasnifu 10 za uzamili na uzamifu katika fasihi simulizi na fasihi andishi ya Kiswahili.

Tangu mwaka wa 2016 amekuwa miongoni mwa wahariri wa Mwanga wa Lugha; Jarida la Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika linalochapishwa kila mwaka.

Dkt. Hamisi Babusa ni mhadhiri wa Kiswahili na Ufundishaji Lugha. Amefunza katika vyuo vikuu vingi vikiwemo Chuo Kikuu cha St. Lawrence, kilicho Canton, NY, Marekani. Kwa sasa ni mhadhiri na Mkuu wa Kitengo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mbali na kuwa mhadhiri, Dkt. Babusa pia ni mwandishi kazi za kibunilizi na za Kitaaluma. Ameandika kazi anuwai kama vile Kamusi Teule na pia A Dictionary of English and Swahili Equivaleny Proverbs na nyingine nyingi.

Amechangia katika mikusanyiko mingi ya Hadithi Fupi na Mashairi na pia akahariri kadhaa. Dkt. Babusa pia ameandika novela za watoto kama vile Msururu Wa Binti Kitabu na Msururu Wa Makumba. Yeye ndiye mwandishi wa kwanza kuwahi kutunga hadithi za Kiswahili za Sayansi Bunilizi Msururu Wa Makumba ambazo zilimfanya akapewa tuzo ya kuwa mmoja wa wanasayansi ishirini bora nchini Kenya, Mwaka 2018.

Aidha yeye ndiye mwasisi na Meneja Msimamizi wa BABUSA TV, chaneli ya mtandaoni ya kufunza watoto lugha ya Kiswahili kwa kupitia vikaragosi na nyimbo.

Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/

Twitter: @KiswahiliPrize

Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize for

African-Literature/1534905843433822

Mawasiliano: Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, [email protected] Dr Lizzy Attree, [email protected], Moses Kilolo [email protected].

Leave A Reply