The House of Favourite Newspapers

Uchunguzi Wanaume Waongeza Safari Kukwepa Haya – 4

SAFARI ya makala yetu ya uchunguzi juu ya visa vya wanaume siku hizi kukubuhu kwa visingizio vya: “Niko safarini.” Lengo likiwa ni kukwepa usumbufu kutoka kwa michepuko inaendelea.

 

Katika uchunguzi wetu tumebaini kuwa uhusiano mwingi uliokuwa kwenye mwaka 2015 sasa hivi imebaki historia na wengi kati yao hawawasiliani kabisa.

 

Ni kama wingu limepita katika uhusiano wa kimapenzi hasa ule uliokuwa umejikita katika anasa na kuonesha mbwembwe za: “Mnatuona?”

Ndoa nyingi zimesambaratika, hasa zile ambazo zilikuwa zinaonekana kuwa na hali bora ya kimaisha.

Ni wagumu na wenye mapenzi ya kweli ndiyo waliobaki wakitetea ndoa na uhusiano wao, tutakuja kuliangazia hili wakati mwingine.

 

Lakini kama tulivyosema wiki iliyopita wanawake wengi katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wajasiriamali wakiwemo mastaa ambao zamani ilikuwa vigumu kuwaona wakiamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli zao kujitafutia.

Kwa mfano; Miss Tanzania 2016, Wema Sepetu siku hizi anajihusisha na biashara za kuuza nguo, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ amepiga hatua kwenye masuala ya mgahawa, Aunt Ezekiel anafanya biashara ya kuuza vinywaji vikali hali kadhalika Irene Uwoya.

 

Kwa uchache hawa ni wanawake mastaa ambao wameamua kuachana na hali ya kutegemea maisha ya ‘kufugwa’ na sasa wameamua kuruka kwa mbawa zao.

Kama alivyosema Kaonga wa Chamazi wiki ilyopita: “Haya ni mapinduzi makubwa ya kifikra kwa upande wa wanawake.”

 

Naamini utakuwa unamkumbuka msichana Veronica ambaye tulimtambulisha katika sehemu ya pili ya makala haya kuwa, ni miongoni mwa wasichana ambao wameonja machungu ya kuachwa na mwanaume ambaye alikuwa anamhudumia kwa kila kitu.

 

Veronica alishuhudia maisha ya anasa aliyokuwa akiishi na mwanaume huyo ambaye ni mume wa mtu na baadaye alivyokuja kuachwa solemba kutokana na ‘vyuma kukaza’ kwa huyo mwanaume.

Alisema, baada ya kupoteza dira ya maisha aliamua kuungana na rafiki yake na kuamua kufungua mgahawa maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambao ndiyo anaoutegemea hivi sasa kuendesha maisha yake.

 

OFM ilimuuliza Veronica mtaji wa kufungua mgahawa huo aliupata wapi; suala ambalo lilikuwa sehemu ya uchunguzi kwa wanawake wengine ambao nao wanaonekana wanaendesha biashara mbalimbali, ambapo Veronica kwa upande wake alisema:

 

“Mapema nilipobaini kuwa, mapenzi yangu na huyo mwanaume yameanza kupoteza mwelekeo, nilijiongeza kiakili, nikaachana kabisa na mambo ya starehe na kuamua kutumia kila ninachokipata kwa akili huku nikijiwekea akiba.

 

“Mara ya mwisho nilipokutana naye huyo mwanaume nilimwambia kuwa kodi ya nyumba ilikuwa imeisha nikamuomba anilipie.

“Alikubali; lakini tofauti na hapo mwanzo ilichukua muda mrefu sana hadi kunipatia fedha hiyo ya kodi tena kwa usumbufu na wakati mwingine nilikuwa nalazimika kumtisha kuwa nitayaanika mambo aliyonifanyia.

 

“Aliponipatia zile fedha niliamua kuachana na maisha ya Sinza, ikabidi niende maeneo ya Kinondoni Mkwajuni nikatafuta chumba kimoja cha bei nafuu nikapanga.

“Sehemu ya fedha nilizokuwa zimebakia pamoja na zile ambazo nilikuwa najiwekea ndiyo ziliniwezesha kuunganisha na sehemu ya fedha za rafiki yangu na kuanzisha biashara yetu ya mgahawa ambayo kimsingi ‘inalipa’ ingawa si sana.”

 

Wakati Veronica akishuhudia jinsi alivyoweza kupata mtaji wa biashara Najma (si jina halisi) yeye anasema aliuza simu aliyonunuliwa na mpenzi wakati wakiwa kwenye uhusiano na kuamua kuanzisha biashara yake ya kuuza mihogo ya kukaanga kwenye Shule ya Msingi Muungano iliyopo Temeke.

“Niliona mwenzangu amebadilika ghafla visa vikawa haviishi, nikimpigia simu hapokei, tofauti na mwanzo ambapo tulikuwa kila dakika tunawasiliana.

 

“Baadaye nikaamua kuachana naye, nikapata mwanaume mwingine, mapenzi yalianza na moto kweli lakini muda mfupi tu niliona naye ameanza kubadilika, ile hali ya kujali ikawa haipo tena ukimlilia shida ndiyo kama umemwambia asikupokelee simu.

 

“Mwisho nikasema siwezi kuishi kwa kutegemea huruma ya wanaume.

“Ikabidi niuze simu yangu aina ya Tekno w5, nikapata hela, nikanzisha biashara zangu, nashukuru maisha yanakwenda ingawa mwanzo ilikuwa vigumu kuanza biashara hiyo kwani nilihisi kama najiaibisha.”

 

Najma anasema, alilazimika kuachana na ile hali ya kujipodoa kila wakati na kuwa mtu wa jikoni akikaanga mihogo, moshi ukawa sehemu ya manukato yake lakini hilo halikumpa shida kwa kuwa alijua anachokitafuta katika maisha yake.

 

Ni biashara hiyo ndiyo iliyomfanya Najma amudu kujiunga kwenye vikundi vya kukopeshana maarufu kama Vikoba ambavyo vimemuwezesha kukuza mtaji wake na kuweza kununua kiwanja ambapo hivi sasa ana mpango wa kuanzisha biashara nyingine ya saluni.

 

Usikose kufuatailia makala haya wiki ijayo ambapo tutaangazia namna ambavyo mbali na wanaume kukwepa michepuko yao hali katika familia zao nayo si salama.

 

Stori: Mwandishi Wetu, Ijumaa Wikienda

Comments are closed.