The House of Favourite Newspapers

Uending Love (Penzi lisilokuwa na mwisho)-42

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao. Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Najua utanifikiria vibaya Jafet kwa sababu niliondoka bila kukuaga, naomba uelewe kwamba bado nakupenda na sikuwa na cha kufanya kutokana na mazingira yalivyokuwa, naumia sana ndani ya moyo wangu kuwa mbali na wewe, siwezi kuzificha hisia zangu,” Anna aliyekuwa amekaa kwenye bustani nzuri ya maua shuleni hapo, alikuwa akizungumza mwenyewe kama mwendawazimu huku akilia kwa uchungu kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.

“Unazungumza Kiswahili? Halafu mbona unalia jamani, kuna tatizo? Unaongea na nani kwani?” sauti ilisikika pembeni ya Anna. Haikuwa kawaida kumsikia mtu akizungumza Kiswahili chuoni hapo, wanachuo wengi walikuwa ni kutoka mataifa ya Ulaya na Asia, Anna akashtuka na kuinua uso wake.

Macho yake yakagongana na ya kijana mtanashati, aliyekuwa amesimama pembeni yake huku akionesha kumshangaa. Anna hakujibu kitu zaidi ya kuyakwepesha macho yake, akaendelea kujiinamia. Alibaki akijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu mtu huyo.

Anna alitegemea kwamba kitendo chake cha kumnyamazia mtu huyo na kukataa kumuonesha ushirikiano kitamfanya aondoke lakini haikuwa hivyo. Alionesha kuguswa na hali aliyokuwa nayo Anna, akamuinamia pale chini alipokuwa amekaa.

“Dada tafadhali nakuomba unyamaze kisha unieleze kinachokusumbua,” alisema kijana huyo kwa upole huku akimgusa Anna begani. Kitendo hicho kilikuwa sawa na kumuongezea uchungu kwani sasa alianza kulia kwa kugugumia, kijana huyo akawa anaendelea kumbembeleza kwa upole.

Baada ya kazi kubwa, Anna alinyamaza lakini kamwe hakuwa tayari kumwambia kilichosababisha akawa kwenye hali hiyo.

“Kwani na wewe unatokea Tanzania?”

“Ndiyo, nyumbani ni Mwanza.”

“Nimefurahi sana kukutana na wewe japo hutaki kuniambia ni kitu gani kinachokuliza. Naitwa William Mbawala, mtoto wa Mheshimiwa Kassim Mbawala, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, nasomea sheria hapa St. Columbus huu ni mwaka wangu wa pili, wewe unaitwa nani?”

“Naitwa Anna, baba yangu ni mfanyabiashara tunaishi jijini Mwanza, Tanzania. Ndiyo kwanza nimekuja kuanza masomo ya usimamizi wa biashara,” alisema Anna huku akijifuta machozi na kamasi.

“Kwa hiyo umetoka Tanzania moja kwa moja?”

“Ndiyo.”

“Hapa Marekani huna ndugu?”

“Hapana sina ndugu na wala hakuna mtu ninayemjua.”

“Mimi wazazi wangu wapo hapahapa nchini Marekani, tunaishi New York, kama hutajali naomba niwe mwenyeji wako,” alisema kijana huyo aliyeonesha kumchangamkia Anna kama watu waliofahamiana siku nyingi zilizopita.

Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kumfanya Anna asahau matatizo yake kwa muda huo, wakawa wanapiga stori za hapa na pale huku kijana huyo akimueleza Anna mambo mbalimbali kuhusu chuoni hapo. Huo ukawa mwanzo wa wawili hao kufahamiana.

***

Taarifa kwamba Anna amesafiri kuelekea nchini Marekani kimasomo, zilimfanya Jafet ashindwe kuzizuia hisia zake, akaanza kumwaga machozi hadharani, akiwa ni kama haamini alichoambiwa. Alibaki amesimama palepale pembeni ya geti, machozi mengi yakiendelea kumtoka huku akihisi uchungu wa hali ya juu.

“Nimekukosea nini Anna mpaka uondoke bila kuniaga? Kama kuna jambo nimewahi kukukosea kwa nini usiniambie ili nikuombe msamaha, oooh maskini mimi,” Jafet aliongea kwa sauti huku akiendelea kulia kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Mlinzi wa nyumba hiyo aliyekuwa upande wa ndani wa geti, alitingisha kichwa kama ishara ya kumsikitikia kijana huyo mdogo kwani alikuwa ni shahidi wa jinsi alivyokuwa na mapenzi ya dhati kwa Anna.

“Wanaume hawalii Jafet, jikaze rafiki yangu,” alisema mlinzi huyo, sauti iliyopenya vizuri kwenye ngoma za masikio ya Jafet, akawa ni kama amemuongezea uchungu zaidi.

Jafet akawa anaendelea kulia kwa uchungu huku akilitaja jina la Anna, hata nguvu za kuendelea kusimama zilimuisha, akasogea pembeni na kukaa chini huku akijalizimisha kuamini kwamba alichokisikia hakikuwa kweli. Baada ya kukaa kwa muda mrefu pale chini, aliinuka na kuanza kujikongoja kuelekea stendi ya mabasi kwani alijua kama atachelewa na kukosa usafiri, hatakuwa na sehemu ya kulala.

Akawa anatembea huku akiendelea kulia, hali iliyowafanya watu waliokuwa wanapishana naye kumshangaa, wengine wakawa wanahisi huenda amepatwa na msiba mzito. Alifika stendi na kwa bahati nzuri akapata usafiri, safari ya kuelekea Rwamgasa, kijijini kwao ikaanza.

Safari aliiona ndefu kuliko kawaida, njia nzima alikuwa akiendelea kumlilia Anna, alijisikia vibaya mno ndani ya nafsi yake, akawa anahisi kama maisha yake yanaelekea ukingoni. Hakuwahi kuwaza hata siku moja kwamba anaweza kuishi bila ya Anna.

Kwa kipindi walichokaa pamoja, tangu wakiwa shule ya sekondari, na mapenzi mazito waliyokuwa wanaoneshana, kwa pamoja vilimfanya Jafet aamini kwamba Anna ndiyo uhai wake. Hakuwahi kufikiria hata mara moja kwamba inaweza kuja kutokea msichana huyo akaenda mbali naye.

“Mbona macho yamevimba hivyo? Halafu siyo kawaida yako kwenda Mwanza na kurudi siku hiyohiyo, nini kimetokea leo?” mama yake Jafet alimuuliza mwanaye huyo muda mfupi baada ya kuwasili kijijini Rwamgasa.

Badala ya kujibu maswali aliyoulizwa, Jafet alianza upya kuangua kilio kwani maswali ya mama yake yalienda kumtonesha mtima wake. Mama yake akabaki amepigwa na butwaa kwani hakujua nini kimemtokea mwanaye mpaka awe kwenye hali hiyo.

Kila alipokuwa anajaribu kumbembeleza ili amwambie amepatwa na nini ndivyo Jafet alivyokuwa anazidi kulia, ikabidi amuache kwa muda, Jafet akaenda kujifungia chumbani kwake ambapo aliendelea kulia mpaka alipopitiwa na usingizi.

Siku hiyo ikapita lakini bado Jafet hakuweza kuzungumza chochote na mama yake. Hata chakula kilikuwa hakipiti kooni, ni mpaka siku tatu zilipopita ndiyo angalau kidogo akaanza kuzungumza.

“Mimi si nilikwambia ukawa huamini mwanangu? Hakuna mapenzi kati ya maskini na tajiri, kama ni mke wa kuoa umri wako ukifika utachagua maskini mwenzako hapahapa kijijini utamuoa, wala huna sababu ya kung’ang’ania mambo makubwa usiyoyaweza,” alisema mama yake Jafet.

Japokuwa alikuwa akimpa maneno ya kumtia nguvu, ndani ya moyo wake na yeye aliumia mno kwa kilichotokea hasa kutokana na ukweli kwamba Jafet alikuwa amejitolea figo kwa ajili ya kumsaidia msichana huyo.

 

 

Leave A Reply