The House of Favourite Newspapers

Uganda Yafungua Mipaka, Yaruhusu Watalii Kuingia

0

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ametangaza kulegeza masharti ya kudhibiti ugonjwa wa corona — Covid-19 — kwa kufungua mipaka ya kimataifa na kuruhusu utalii kurejea. Aidha raia wa Uganda wanaorejea kutoka nje ya nchi watalazimika kujitenga nyumbani kwa muda wa siku 14.

 

Akihutubia kupitia matangazo ya televisheni siku ya Jumapili, Museveni amesema wageni wanaowasili nchini humo wanalazimika kufanya vipimo vya corona, saa 72 kabla ya kuwasili. Nyumba za ibada zimefunguliwa lakini idadi ya waumini imetakiwa kutozidi watu 70.

 

Hata hivyo,  wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi, sekondari na taasisi za ufundi na biashara watafungua shule katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu. Museveni amesema madarasa mengine yatafunguliwa Januari mwakani.

 

Vilevile, makatazo ya kuzuia usafiri wa umma na binafsi yameondolewa. Michezo ya nje imeruhusiwa kurejea, lakini haitakuwa na mashabiki. Wachezaji walikuwa katika msimu wa kujitenga na wanapaswa kuwa wamepimwa saa 72 kabla ya michuano katika kila wiki mbili.

 

Makatazo mengine kama zuio la mikusanyiko ya umma na kutembea usiku kuanzia saa tatu hadi 12 asubuhi litaendelea. Pia  amelegeza masharti ya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19, licha ya maambukizi ya ugonjwa huo kuongezeka na kufikia 6,287, huku vifo vikifikia 63.

Leave A Reply