The House of Favourite Newspapers

Ugando ni habari nyingine Simba SC

0

PicsArt_1448539024769Kinda wa Simba, Hija Ugando.

Na Hans Mloli,
Dar es Salaam
SIMBA inaonekana kuanza kukaa sawa na kuzitetemesha timu zilizopo kileleni lakini pia inazidi kuibua watu wapya kila kukicha, baada ya Danny Lyanga sasa inaonekana ni zamu ya kinda Hija Ugando ambaye alishangaza kwa kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya African Sports, juzi Jumamosi.
Ugando ambaye alisajiliwa na Simba katika dirisha dogo la usajili la Desemba, mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitatu chini ya benchi la ufundi la Dylan Kerr, alifanikiwa kucheza kwa ustadi na kusababisha mabao mawili kati ya manne yaliyofungwa siku hiyo.
Aidha, tangu Ugando asajiliwe kikosini hapo, hakuwahi kuitumikia timu hiyo kabla katika mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara zaidi ya kucheza kwa dakika 70 katika mechi dhidi ya Jamhuri ya Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi lililomalizika hivi karibuni visiwani humo. Nyingine ni ile ya Kombe la FA dhidi ya Burkina Faso ya Morogoro.
Lakini kwa mara ya kwanza alipoaminiwa na kocha anayekaimu nafasi ya kocha mkuu kwa sasa kikosini hapo, Mganda, Jackson Mayanja katika mchezo huo, alionyesha kiwango cha juu na kuisumbua vilivyo ngome ya ulinzi ya wapinzani wao.
Ugando alikabidhiwa majukumu ya kiungo wa kulia akisaidiana vilivyo na washambuliaji Ibrahim Ajib na Mganda, Hamis Kiiza aliyefunga mabao mawili na kufikisha jumla ya mabao 12 tangu kuanza kwa msimu huu.
Ugando ambaye alianza kuonyesha cheche zake tangu mwanzo wa mchezo huo, alipiga krosi kadhaa hatarishi kwenye lango la wapinzani na mbili kati ya hizo zilitua miguuni mwa Kiiza na Ajib ambapo kama wangekuwa makini wangefunga.
Hata hivyo, wakati Simba inaongoza kwa mabao 2-0, Ugando alisababisha bao la tatu baada ya kumwekea pasi safi ya mwisho Kiiza ambaye hakufanya makosa zaidi ya kutupia wavuni. Ugando hakuishia hapo kwani alihitimisha karamu ya mabao siku hiyo kwa kufunga bao la nne baada ya kugongeana vizuri na Mwinyi Kazimoto kabla ya kupenya ndani ya 18 na kumchambua kipa.
Si kushambulia tu, Ugando ambaye alitoka dakika ya 77 mapema baada ya kufunga bao na kumpisha Musa Mgosi, alionyesha pia uwezo mkubwa wa kupokonya mipira kwa maadui na kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza.
“Nimefurahi nimecheza vizuri kwenye mechi yangu ya kwanza ya ligi na kufanikiwa kufunga bao, tangu nimefika sijawahi kukaa hata benchi katika mechi za ligi lakini leo (juzi) nimepata nafasi ya kuanza moja kwa moja,” alisema Ugando.
Kwa upande wa Mayanja, alisema: “Ugando ni kijana mzuri na amejitahidi kweli lakini bado anahitaji kuongeza bidii na kufanya kazi kwa nguvu ili azidi kuwa zaidi ya hapa.”

Leave A Reply