The House of Favourite Newspapers

Ujambazi wa Kushangaza Shinyanga

0

kamugishaKamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha

SHINYANGA, Kahama: Hii kali. Ujambazi wa aina yake unaoshangaza umetokea wiki iliyopita eneo la Majengo Sokola wilayani hapa, baada ya majambazi kuvamia nyumba ya mkazi mmoja na kuvunja dirisha lake kwa kutumia vifaa aina ya tindo na nyundo usiku wa manane.

Tukio hilo lililotokea majira ya saa saba na nusu usiku, linadaiwa kutekelezwa na majambazi hayo yapatayo nane, ambayo wakati yakivunja dirisha hilo, yalimweleza mwenye nyumba Nkanda Charles, aliyekuwa akipiga kelele za kuomba msaada, kuwaandalia kabisa fedha.

Habari zinasema kufuatia kelele hizo, majirani walitoka ili kwenda kutoa msaada, lakini walijikuta wakikwama baada ya majambazi hayo kufyatua risasi hewani ili kuwatisha, kitu kilichofanya wafanye kazi yao bila bughudha yoyote.

Baada ya majambazi hayo kufanikiwa kuling’oa dirisha hilo na kulisukumia ndani, mwenye nyumba huyo na mkewe walikimbilia sebuleni ambako walipata upenyo wa kukimbia, lakini kabla hajafika mbali, majambazi hayo yalimpiga risasi mguuni. Kisha waliingia ndani ambako walichukua simu inayotumika kwa matumizi ya M Pesa ikiwa na shilingi laki tatu ndani, pamoja na shilingi laki moja taslimu iliyokuwa mezani.

Akizungumzia tukio hilo, Nkanda alisema majambazi hayo yalifika nyumbani kwake na kumgongea dirishani, wakimtaka kuwaandalia pesa kwani walizihitaji kabla hawajaanza kulivunja dirisha lake na kuliangushia ndani.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Mary Sumuni na Diwani wa Kata Benard Mahongo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo ni muendelezo wa matukio ya kihalifu yanayoendelea kuikumba Kanda ya Ziwa.

Leave A Reply