The House of Favourite Newspapers

Viongozi Walaani Shambulio Dhidi ya Kituo cha Nyuklia Ukraine

0

Kumekuwa na kilio cha kimataifa kuhusu shambulio lililotokea usiku la Urusi kushambulia kituo kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya, huko Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine.

 

Shambulio hilo lilisababisha jengo la utawala kushika moto, lakini mtambo wenyewe uko salama – ingawa chini ya udhibiti wa Urusi.

 

“Vitendo vya hatari vya Rais Putin sasa vinaweza kutishia moja kwa moja usalama wa Ulaya yote,” Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema.

 

“Sio tu hatari kwa Ukraine na Warusi, ni hatari kwa Ulaya na inacheza na moto ambao kwa kweli hauna umuhimu au ulazima wowote,” Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace ameongeza.

 

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema “mashambulizi ya kutisha” kutoka Urusi “lazima yasitishwe mara moja”, huku Rais wa Marekani Joe Biden ameitaka Moscow kusitisha shughuli zake za kijeshi katika eneo hilo.

 

Jens Stoltenberg, mkuu wa Nato, anasema shambulio hilo linaonesha “kutojali kwa vita hivi na umuhimu wa kuvimaliza”.

 

Taarifa ya Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi inalaani “shambulio hilo baya” kama “shambulio dhidi ya usalama wa kila mtu” na kutoa wito kwa EU “kuendelea kuitikia kwa umoja na azma kubwa” kuiunga mkono Ukraine.

 

Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store pia amelaani vikali kwa shambulio hilo. “Aina hii ya shambulio ni wazimu,” amesema.

Leave A Reply