The House of Favourite Newspapers

Ukraine Yadai Kumuua Kamanda Mwingine Wa Urusi

0

Ukraine imedai leo kuwa vikosi vyake vimemuua kwa kumpiga risasi Kamanda wa Jeshi la Maji wa Urusi, Andrey Paliy mwenye umri wa miaka 51, tukio ambalo linatajwa kuwa pigo kubwa kwa vikosi vya Rais Vladimir Putin.

 

Paliy aliyekuwa kiongozi msaidizi wa msafara wa meli za kivita za Urusi katika Bahari Nyeusi, anatajwa kuwa ndiye afisa mkuu pekee wa jeshi la wanamaji anayedaiwa kuuawa katika vita nchini Ukraine, ingawa Kyiv inadai kuwaua majenerali watano wa jeshi hilo mpaka sasa.

 

Inaelezwa kwamba kamanda huyo amepigwa risasi katika mapigano jirani na Mji wa Bandari wa Mariupol ingawa hakuna taarifa zaidi zinazoeleza amepigwa risasi katika mazingira gani.

Serikali ya Moscow haijatoa tamko kuthibitisha au kukanusha taarifa za kamanda huyo kuuawa ingawa inaelezwa kwamba rafiki yake wa karibu Konstantin Tsarenko ambaye ni Katibu wa Halmashauri ya Chuo cha Askari wa Majini cha Sevastopol Nakhimov amethibitisha taarifa hizo.

 

Gazeti la The Sun limemnukuu afisa wa juu nchini Ukraine, Anton Geraschenko akieleza taarifa za kuuawa kwa Paliy, leo Jumapili ingawa hakutoa taarifa zaidi.

 

Paliy alizaliwa nchini Ukraine katika Jiji la Kyiv lakini mwaka 1993, alikataa kujiunga na jeshi la Ukraine na badala yake akachagua kwenda kujiungana Jeshi la Urusi kamandi ya wanamaji.

 

Madai hayo ya Ukraine, yanakuja muda mfupi baada ya Urusi kudai kwamba imewaua takribani wanajeshi 100 wa Ukraine pamoja na mamluki waliokuwa wakiwasaidia baada ya kupiga makombora katika chuo kimoja cha mafunzo ya wanajeshi wa kigeni nchini humo.

 

Mpaka sasa, Ukraine inadai kuwaua makamanda wa ngazi za juu wapatao watano tangu kuanza kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.

 

Wengine waliouawa ni Kanali Sergei Sukharev wa Kikosi cha 331 cha Askari wa Parachute kutoka Kostroma, ambaye aliuawa Machi 18, mwaka huu na Andrei Sukhovetsky mwenye umri wa miaka 47 ambaye aliuawa wakati wa operesheni maalum ya mdunguaji mnamo Machi 3.

 

Pia yumo Meja Jenerali Oleg Mityaev mwenye umri wa miaka 47, aliyekuwa kamanda wa kitengo cha askari wa miguu wa kikosi cha 150 ambaye aliuawa katika mapigano karibu na mji uliozingirwa wa Mariupol.

 

Meja Jenerali Vitaly Gerasimov mwenye umri wa miaka 45, yeye aliuawa mnamo Machi 7 nje ya mji wa mashariki wa Kharkiv na Kanali Andrey Kolesnikov, Kamanda wa Kikosi cha Vifaru cha Kantemirovskaya naye aliuawa katika mapigano mnamo Machi 11.

Leave A Reply