The House of Favourite Newspapers

Ukweli mtu aliyekamatwa na kichwa cha mtu

0

KichwaaaNa Mwandishi Wetu, AMANI

Mbeya: Taharuki Imezuka mjini hapa baada ya kuenea kwa picha za mtu (pichani) anayedaiwa kukamatwa mkoani Mbeya akiwa anatembea mitaani na kichwa cha mtu aliyechinjwa muda mchache, Amani limechimba na kubaini ukweli.

Katika tukio hilo la kutisha lililoteka hisia za wengi wikiendi iliyopita, mtu huyo anaonekana pichani akiwa amekibeba kichwa hicho huku akikatiza mitaani bila wasiwasi na wengi walisema lilitokea jijini Mbeya bila kutajwa wilaya au eneo kamili.

Baadhi ya wachangiaji wa picha za mitandaoni wakaanza kusema kuwa, Mbeya umeanza tena, wakikumbushia wakati wa mauaji ya watu kuchunwa ngozi mkoani hapa.

Baada ya kushuhudia picha hizo huku jeshi la polisi likiwa halijatoa tamko, Amani lilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo kama kweli lilijiri mkoani Mbeya.

Hivyo Amani juzi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Kidava Shali ambaye alikanusha kutokea kwa tukio hilo mkoani mwake huku akilaani upotoshwaji wa taarifa na kuwatia hofu wananchi jambo ambalo wao kama jeshi alisema hawako tayari kuwafumbia macho wapotoshaji na wanaendelea na uchunguzi kumbaini aliyesambaza taarifa hizo.

“Huo ni upotoshaji mkubwa kwa umma. Ni kuwatia hofu wananchi. Tukio hilo siyo la Mbeya. Na niwatake wananchi kuwa makini na taarifa wanazozipata na kuanza kuzisambaza bila kujua ukweli wake. Tunaendelea na uchunguzi kubaini aliyeeneza uvumi huo,” alisema Kidava.

Hata hivyo, Amani lilipochimba zaidi ilibainika kuwa, tukio hilo lilitokea nchini Nigeria na siyo Mbeya wala Tanzania kama ilivyoenezwa na watu wasiofahamika na kusababisha taharuki kubwa.

Kwa mujibu wa Mitandao ya Gistmania na Freshloaded, tukio hilo lilijiri nchini Nigeria likimhusisha jamaa huyo kutoka kwenye jamii ya watu wa Hausa.

Ilielezwa kwamba, kichwa hicho alichokamatwa nacho mwanaume huyo kilisadikiwa ni cha binamu yake (mtoto wa mjomba’ke) na alimchinja kwa lengo la kujipatia fedha. Hata hivyo, mtu huyo alitiwa mbaroni kupisha uchunguzi wa polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

Leave A Reply