Ukweli Pete ya uchumba ya Nandy

BAADA ya utata kuibuka kutokana na mwanamuziki William Lyimo ‘Billnass’ kumvisha pete ya uchumba, mpenzi wake ambaye pia ni mwanamuziki mwenzake, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, ukweli umeanikwa, IJUMAA WIKIENDA linakupa habari kamili.  Billnass alimvisha Nandy pete hiyo ndani ya kipindi kinachorushwa kupitia Televisheni ya ETV ambapo baadhi ya watu walidai kuwa inawezekana ni maigizo siyo halisi.

Watu hao walihoji kuwa inawezekanaje pete ya uchumba wakavishane kwenye shoo bila kuwepo kwa wazazi wa pande zote mbili? Hivyo inawezekana ikawa ni kiki tu.

“Naona kabisa hii ni kiki, maana hakuna pete ya uchumba ambayo mtu anavalishwa kwenye shoo hata siku moja kwa sababu hiyo ni hatua mojawapo kubwa ya kuelekea kwenye ndoa, sasa kama ni ‘surprise’ maana hata wazazi hawana taarifa yoyote ile, kitu ambacho siyo sawa,” alisema shabiki mmoja.

UKWELI NI HUU

Ili kuujua ukweli wa pete hiyo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Nandy ambaye alisema kuwa, alikuwa hajui kama angevalishwa pete siku hiyo, ilikuwa ni ‘sapraizi’ kwake licha ya kwamba huko nyuma aliwahi kukiri kuwa ana mpenzi na wako mbioni kufunga ndoa ambaye ndiye huyo.

“Hii ni pete ya ukweli siyo kiki kama wengi wanavyosema, sikujua kama nitavishwa pete, lakini kama mlinifuatilia zamani nilisema kuwa nina mtu na ni kwamba tuna matarajio ya kufunga ndoa na pia watu wameshajua ni nani, basi mimi nashukuru,” alisema Nandy.

Kwa muda mrefu, Nandy na Billnass wamekuwa wakikanusha kuwa kwenye uhusiano baada ya kutengana mwanzoni na kila mmoja kuchukua hamsini zake, lakini sasa ni wachumba rasmi.

STORI: IMELDA MTEMA, DAR


Toa comment