The House of Favourite Newspapers

Umeya Jiji la Dar Wapigwa Kalenda

0
1Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Jiji, Gaston Makwembe (kushoto).
HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imeahirisha uchaguzi wa meya wa Jiji uliokuwa ufanyike leo, mpaka hapo tarehe itakapotangazwa baadaye.
Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Jiji, Gaston Makwembe alisema uchaguzi huo uliokuwa ufanyike leo saa nne asubuhi katika ukumbi wa Mmikutano wa Karimjee, umeahirishwa.
Alisema tarehe ya uchaguzi huo itapangwa baadaye na taarifa zitatolewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari bila kueleza sababu ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM ) kinawakilishwa na Diwani wa Kinondoni, Yusuph Omary Yenga, Ukawa kwa mwamvuli wa Chadema wanawakilishwa na Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita, huku mgombea wa nafasi ya Naibu Meya akitarajiwa kutoka CUF.
Awali, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitoa wito kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia uchaguzi huo kwa amani na haki ili usifanyike kama wa kumtafuta meya wa Ilala na Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi.
Leave A Reply