The House of Favourite Newspapers

Unachezea Bahati wenzako Wanaitamani

0

NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha kwenye ukurasa huu, ni matumaini yangu kwamba umzima wa afya na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku. Wiki iliyopita tulianza kuijadili mada hii kama inavyojieleza hapo juu, kwamba unapopata bahati ya kupendwa, usiichezee kwa sababu kuna wenzako wanaitamani.

Ni makosa makubwa sana kumfanyia mwenzi wako vituko eti kwa sababu tu unajua anakupenda. Unapoona wa kazi gani, kuna wenzako wanampigia mahesabu watampata lini na hii inawahusu wote, wanawake na wanaume. Mwingine akishapendwa basi hujiona mzuri yeye, anahisi hata akiachana na wewe atatokea mwingine na kumpenda, tena zaidi ya ulivyompenda!

Atakudharau kwa sababu ya hali yako duni akiamini anaweza kupendwa na mabosi au watu maarufu! Sitaki msomaji wangu uje kutafuta shuka wakati kumeshakucha! Akikuonesha anakupenda na wewe mlipe upendo wa dhati, ukifanya hivyo maumivu ya mapenzi utayasikia tu lakini ukimfanyia makusudi, siku akiondoka ndipo utakapokuja kutambua thamani yake lakini tayari itakuwa ‘too late!’

Ipo kasumba ya baadhi ya watu, wanapokuwa kwenye hatua za mwanzo za uhusiano wao, wanakuwa wapole, wenye heshima na nidhamu kwa wenzi wao, mambo ambayo kimsingi ndiyo yanayojenga mapenzi ya dhati.

Inawezekana ukawa umeingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hakupendi kiivyo lakini kwa sababu ya upweke au sababu nyingine yoyote, akaamua kukupa nafasi kwenye moyo wake. Sasa wengi huwa makini sana kwenye hatua za mwanzo kama nilivyoeleza.

Mtu yeyote, hata kama hakuwa anakupenda sana, ukimuonesha kumjali, kumpenda kwa dhati, kumheshimu na kumtimizia haja zake vizuri, ni lazima atakupenda tu. Upo ushahidi wa watu ambao waliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na watu ambao hawakuwa wakiwapenda lakini wakajikuta wakizama mno kimapenzi kutokana na mambo wanayofanyiwa na wenzi wao.

Kwa hiyo tunachojifunza hapa, ni kwamba mapenzi ni hisia na hisia hizo siyo za mara moja, lazima ziwe endelevu ili mapenzi yadumu. Kuzifanya hisia zidumu, ni lazima ufanye yale mambo ambayo yanazalisha mapenzi ndani ya moyo wa mwenzi wako. Isiwe kwa sababu ameshakupa nafasi ndani ya moyo wake, ameshakuzoea na kukupenda kwa sababu ya yale uliyomuonesha siku za mwanzo, basi unaanza kumdharau, unaamini kwako hapindui na hawezi kupata mwingine kama wewe.

Unautesa moyo wake kwa makusudi, anakupigia simu lakini hupokei na hata ukiona missed call hupigi, anakutumia meseji lakini hujibu na hata ukijibu, ni kwa muda unaoutaka mwenyewe bila kuwa na sababu zozote za maana. Hutaki kuwa naye karibu tena, wewe muda wote uko bize na kazi, marafiki au upo bize na simu ukichati kwenye mitandao ya kijamii.

Huzijali tena hisia zake, hujali tena upendo wake, unaamini kwako ameshafika na hana tena ujanja! Kama na wewe ni miongoni mwa watu wenye kasumba hii, nakushauri chukua hatua kabla hujalia wewe kwa sababu unapomtesa mwenzako na kumfanya alie, machozi yake hayawezi kwenda bure, lazima yatakurudia.

Ukimpata mtu anayekupenda na kukujali, hiyo ni bahati ambayo unatakiwa kuing’ang’ania. Usiichezee kwa sababu watu watu wengi wanaokuzunguka, ambao wanatamani wao ndiyo wangekuwa hapo ulipo wewe. Wanatamani wao ndiyo wangemmiliki huyo uliyenaye. Kuwa makini, mpende na muoneshe kwa vitendo kama unampenda. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri

Leave A Reply