The House of Favourite Newspapers

UNAOMBAJE MSAMAHA KWA MPENZI WAKO ?

MARAFIKI karibuni katika safu yetu hii ya XXLove ambayo hutupa maarifa kuhusu uhusiano na mapenzi. Siku zinayoyoma, zimebaki siku chache kuifikia Sikukuu ya Krismasi na hatimaye Mwaka Mpya wa 2019. Je, umejiandaaje na sikukuu hizi za mwisho wa mwaka? Unalo jipya au ndiyo unaishi kimazoea? Ushauri wangu kwako, ufanye mwaka huu wa tofauti kwako. Jiandae vema kiuhusiano ili umalize mwaka na mwandani wako kwa furaha.

Katika kipindi hiki cha sikukuu, msiwe mbalimbali. Jengeni uhusiano wenu kwa kujadiliana changamoto zilizowakabili katika mwaka huu ili mtakapoanza mwaka mpya, muwe wa tofauti kabisa. Yes! Sasa turejee katika mada yetu ya leo. Nazungumzia kuhusu msamaha. Ndugu zangu, kukosea katika maisha ya binadamu ni kawaida. Ni sehemu ya maisha yake. Tena inaaminika kwamba, kukosea ni kujifunza, maana kosa utakalofanya leo ni funzo la kesho.

Hakuna cha ajabu. Ni kawaida kabisa, lakini jambo la msingi ni kwa namna gani tunajifunza kupitia makosa? Ni kwa jinsi gani tunamaliza tofauti hizo? Maana unaweza kuwa hodari wa kukosea au ukawa bingwa wa kusamehe, lakini wimbo huo ukaendelea kubaki hivyohivyo kila siku. Lakini pia, wapo ambao kwa bahati mbaya, bila matarajio yao wanajikuta wakiwa wamewaudhi wapenzi wao. Ni bahati mbaya na yawezekana kabisa wanaumia sana mioyoni mwao, lakini wakashindwa jinsi ya kumaliza ‘bifu’ hilo katika penzi lake.

Siku zote mkosewa hukosa raha, hupoteza hamu ya kukutana na mpenzi wake, lakini kubwa zaidi, hujishusha, hukushusha thamani ya mapenzi yake kwako. Lakini mkosewa huyo huyo, akioneshwa kwamba makosa yaliyofanyika hayakuwa ya makusudi na kutumia njia bora za kufikisha hisia zako kwake, hujisikia amani na hali yake kurejea kawaida.

Hapa naita ni ushawishi wa kuomba msamaha. Huwezi kujua njia bora ya kuomba msamaha kama utakosa kitu kinachoitwa ushawishi. Rafiki zangu, yawezekana ukawa upo katika kipindi cha matatizo na mpenzi wako na hujui jinsi ya kuweka mambo sawa. Wakati mwingine huna tatizo, lakini kwa sababu upo kwenye uhusiano, basi si ajabu mambo kwenda mrama siku moja. Hapa chini, nimekuandalia mambo matano muhimu ya kuzingatia unapokuwa umekwenda kinyume kidogo kwa mpenzi wako.

Weka ubongo wako wazi, kuruhusu somo hili kichwani mwako, ambalo litakuwa hazina yako na mwongozo katika uhusiano wako. Kitu kikubwa ukumbuke, kukosea ni kawaida. Inatokea kila siku katika maisha yetu, hilo litoshe kukupa umuhimu wa kufuatilia kwa makini somo hili. Karibu darasani marafiki.

TAFAKARI UKUBWA WA KOSA

Hapa tayari umeshagundua kwamba umemkosea mpenzi wako na ni kweli kwamba unaumizwa sana na kosa lako, lakini kwa sababu hujamwambia chochote, naye hana raha na wewe. Hana amani ya moyo.

Hapa unashauriwa kutulia na kutafakari ukubwa wa tatizo. Kufahamu ukubwa wa tatizo kutakupa muongozo mzuri sana wa jinsi ya kutatua tatizo hilo. Angalia ulimfanyia nini na kwa kiwango gani? Mathalan unaweza kuwa ulimuudhi kwa sababu alikupigia simu zaidi ya mara kumi bila kupokea, akakasirika. Hili ni kosa dogo. Lakini yawezekana alikuta meseji ya mapenzi kwenye simu yako au alikufumania; Haya ni makosa makubwa. Tafakari na ujue ukubwa wa kosa lako.

JUTIA KWA MOYO

Hii ni kwa ajili yako wewe mwenyewe. Rafiki zangu, kutakuwa hakuna maana yoyote kuomba msamaha wa kinafiki au kuomba msamaha ili kumaliza mambo, kama msamaha wako haujatoka moyoni.

Ukiwa peke yako, jiaminishe kwamba umekosea na kwa hakika unahitaji kusamehewa. Jutia ndani ya moyo wako, kwa dhati kabisa ukiwa na ahadi kwamba hutarudia tena. Hili ni zoezi la kisaikolojia ambalo litakusaidia baadaye wakati ukikutana na mpenzi wako kwa ajili ya kuomba msamaha.

Wiki ijayo tutamalizia mada yetu, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

 

Comments are closed.