The House of Favourite Newspapers

Unatafutaje umaarufu ili ufanye utapeli, umalaya?

kim-kardashian.jpgZa Chembe Lazima Ukae

Ojuku Abraham, +255 719 786 355

MIAKA kadhaa ya kufanya kazi na watu wenye majina makubwa, wenye mamlaka na walio katika nafasi nyeti, imenipatia funzo kwamba unapaswa kuwa makini sana kwa nyendo zako, kama lengo lako ni kuwa mtu maarufu, lakini mwenye hadhi katika jamii.

Unapokuwa mtu maarufu, unachukuliwa kama mfano na bahati mbaya, mfano ni mfano tu, uwe mbaya au mzuri. Mtu anaweza kumwambia mwanaye kwa mfano, asiwe malaya kama Kim Kardansian, yule dada mrembo mwenye msururu wa wanaume aliotokanao huko Marekani. Ni staa mkubwa lakini mwenye sifa mbaya, licha ya hivi sasa kuwa mke wa Kanye West.

RonaldoNa mtu mwingine anaweza kukuambia kuwa wapaswa kuwa na nidhamu, heshima na utu kama Ronaldo de Lima, mwanasoka nyota aliyepata kila aina ya mafanikio uwanjani, akishinda mataji yote makubwa ya soka duniani, lakini akibakia kuwa muungwana uwanjani, mpole nje ya uwanja na mwenye utu katika maisha ya kijamii.

Umaarufu unakufanya uwe mtu wa kutazamwa kwa kila unachokifanya. Watu wataulizana, hivi fulani ameoa? Ana watoto wangapi, maisha yake yakoje, anapendeleaga nini na mambo mengine chungu nzima. Na mara nyingi, umaarufu unapatikana kupitia kazi tunazofanya.

Lakini umaarufu huu nao umegawanyika, ule wa sifa mbaya na ule wenye hadhi. Tunao mastaa ambao siku zote tunategemea kusikia juu ya skendo na inapotokea wakatokea kwenye shughuli zenye heshima, kila mmoja huidharau hafla hiyo. Hawa wapo na wote tunawajua.

Lakini wapo baadhi ya mastaa wetu ambao inakuwa vigumu kidogo kuamini tunaposikia habari mbaya zinazowahusu, hata kama ni kweli wamefanya kinachosemwa. Hii ni kutokana na jinsi wao wenyewe walivyojitengeneza katika umaarufu wao.

Enzi zile nikikua, kulikuwa na jambazi mmoja maarufu sana jijini Dar es Salaam, akiitwa Nyau. Habari zake zilitingisha kila kona na kila mmoja aliogopa kukutana naye. Ziliposikika habari kwamba ameuawa, kila mpenda amani alifurahi. Unapoona watu wanafurahia anguko lako, ni dhahiri, maisha yako yalikinzana na matazamio yao!

Kwa nini nimesema hivi, ni kwa sababu uzoefu wangu kwa miaka niliyojihusisha na mastaa, unanionesha kuwa wapo baadhi yao hawajui namna ya kuishi katika hadhi waliyonayo, wengi wao wakitumia ustaa wao kujinufaisha kwa njia zisizofaa na wachache, wakiishi hasa maisha yenye kwenda sawia na hadhi waliyojijengea.

Wapo watu wanaotafuta majina makubwa ili wafanye utapeli na umalaya. Lengo lao ni kutumia umaarufu wa majina yao ili kufanikisha lengo lake. Bahati mbaya inakuja pale anapoitumia fani kutimiza lengo lake, matokeo yake ni kuonekana watu wote walio katika industry kuwa ni wenye sifa kama zake.

“Unataka kuwa muigizaji, achana na hiyo fani, wasichana wa Bongo Movie ni malaya,” mtu mmoja anaweza kumwambia binti anayejaribu kupenyeza ili awe muigizaji, aweze kutimiza ndoto zake za muda mrefu.

Hii haimaanishi kweli kuwa Bongo Movie ni chaka la wahuni, isipokuwa kwa sababu mtu mmoja au wawili, wameitumia fani hiyo vibaya. Watu wengine wamejaribu kuwa wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, dansi au taarab, wakiamini huko kunaweza kupata umaarufu.

Ninajua wapo wasanii wenye majina makubwa, lakini wanayatumia vizuri kuchangamkia fursa zinazokuja mbele yao, hawa sina tatizo nao. Lakini sipendezwi zaidi na matapeli au malaya wanaotumia fani kutekeleza matakwa yao.

Rai yangu ni kwa jamii zinazohusika, kuwakataa watu hawa kuwa miongoni mwao. Tusikubali matapeli wajineemeshe kwa majina wanayoyapata kupitia fani zetu. Uzuri ni kuwa tunajuana, tunafahamu kuwa huyu anaishi kwa sababu ya utapeli au wanaume, fani ni kigezo tu, tumkatae!

Comments are closed.