The House of Favourite Newspapers

Unavyoweza kujipaisha kithamani kwa mpenzi wako!- 4

LEO tupo kwenye sehemu ya mwisho kabisa ya mada hii. Tumeshaona mengi kuhusu namna ambavyo unaweza kujipandisha thamani kwa mpenzi wako.  Tuliona athari kadhaa za kuharakisha faragha. Tuendelee kuona athari nyingine zaidi;

(III) MAPUNGUFU

Ukishautoa mwili wako kwa mwanaume, kama ni aina ya wale ambao huchunguza sana ni rahisi kukutoa kasoro. Kikubwa unachotakiwa kuelewa hapa ni kwamba kuutoa mwili wako hovyo kunakupeleka kwenye kujichoresha na pengine kama umekutana na mwanaume kicheche ataishia kukutumia na kukuacha kama alivyokukuta!

(IV) MSIMAMO

Pamoja na kwamba wanaume wengi ndiyo hasa wanaokuwa wa kwanza kushawishi kupewa mapenzi, ukweli ni kwamba ni wepesi wa kulaumu na kuwaona wenzi wao hawana msimamo na maisha yao. Kukuweka kwenye kundi hilo kutakukosesha nafasi ya uhakika ya kuingia kwenye ndoa, maana wengi wanapenda kuwa na wenzi wenye msimamo thabiti.

(V) MIMBA

Kuna suala la mimba. Nimekutana na kesi nyingi sana za aina hii. Wanaokutana kimwili na wenzi wao bila mpangilio huwa hawazingatii sana suala la mimba, lakini inapotokea ndiyo huanza kuhangaika kutafuta ushauri.

(VI) MAGONJWA

Kuharakia mapenzi kuna matatizo mengi. Ukiacha kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya zinaa, pia kuna suala la ujauzito. Mathalani utakuta msichana amepata mimba isiyotarajiwa, anatafuta shotikati na kwenda kuitoa, hapo kuna matatizo mengine mengi anayoweza kuyapata kutokana na kitendo hicho.

KUWA MSHAURI

Nataka niseme wazi kabisa kwamba wasichana wengi hujidharau na pengine huhisi kuwa hawawezi kuwa na mawazo mazuri kwa wenzao. Sikia nikuambie; kama kuna jambo lenye thamani katika maisha ya uhusiano ni pamoja na kusaidiana mawazo.

Wakati mwingine msichana anaweza kuwa na mawazo mazuri lakini akaogopa kuyatoa kwa sababu tayari yeye si wa thamani tena. Mfano, wasichana wengi wanapenda sana kupiga mizinga kwa wapenzi wao, wengine ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuanzisha uhusiano. Ukiwa namna hiyo huwezi kuwa na thamani.

Nimekutana na kesi nyingi sana za namna hiyo. Wapo wanaoomba ushauri kuwa wapenzi wao hawawatunzi, wakiomba pesa hawawapi; kwani siku zote kabla yake ulikuwa unaishi vipi? Jifunze kuishi kwa kujitegemea. Mwanaume anakuwa na amani zaidi kama akitoa fedha au kumsaidia mpenzi wake kwa uamuzi wake –siyo kuombwa. Tafsiri inayokuwa nyuma yake ni kuhonga. Kama anakuhonga ana haja gani ya kukuweka kwenye ratiba zake za mbele?

ACHA MAISHA  YA VIFICHO

Baadhi ya watu wanapenda kufanya mambo yao gizani. Anaishi maisha ya kificho na wakati mwingine anadanganya maisha yake halisi na kuonesha picha nyingine kabisa mbele ya mpenzi wake. Hili ni tatizo.

Mwanaume ukianza kuonesha dalili kwamba penzi lenu ni la siri au unaficha ukweli wa familia yako n.k, anakutoa thamani. Mwoneshe mwenzako ulivyo. Usifiche mambo yako. Mathalani una tatizo fulani la kimaisha, usimfiche, mwambie mapema.

Kumwambia kutamfanya kwanza aone unampenda, humfichi na una malengo naye ya baadaye. Ni wazi kwamba kama ungekuwa humpendi na huna malengo naye ungemficha maisha yako. Kuwa wazi kutamfanya akupandishe thamani maradufu akijua kuwa amekutana na mtu sahihi. Jitahidi kuwa wazi kwa kadiri uwezavyo ili uendelee kujipandisha thamani zaidi na zaidi.

MSAIDIE

Kipengele muhimu ambacho hudhihirisha mapenzi ya dhati na kuingia ndani kwa haraka zaidi ni kusaidiana. Yapo mambo mengi ya kusadiana, lakini najua wengi mmekwenda moja kwa moja kwenye fedha. Msaada au kusaidiana siyo kwenye fedha pekee. Kati ya mambo ya msingi zaidi ya kumsaidia mwenzako ni pale anakupokuwa mhitaji. Mathalani anaweza kuwa na tatizo na fedha, lakini lazima ujiulize ni kwa ajili ya nini?

Usije ukampa fedha ya kwenda disko au kulewa baa ukadhani utakuwa umejipandisha thamani, la hasha! Nazungumzia juu ya mambo ya msingi kabisa ambayo mwenzako atayambuka siku zote na kukuzidishia thamani yako.

Jitahidi kumsaidia kadiri unavyoweza utakuwa juu kithamani, si tu kwamba ataona penzi lako la dhati kwake bali pia atafahamu kuwa mwanamke aliyenaye si wale wa kusubiri kupelekewa tu! Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

 

Comments are closed.