The House of Favourite Newspapers

Unawezaje Kuitibua Ndoa Yako kwa Uvaaji wa Kisasa?

0

MAKALA: Na Amran Kaima | RISASI JUMATANO

NI wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Kwa upande wangu namshukuru Mungu kwa kunijaalia siha njema kiasi cha kuniwezesha kuwa nanyi tena kupitia safu hii ambapo tunaelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu.

Wiki hii nataka kuzungumzia suala la mavazi hasa kwa watu walio kwenye ndoa. Bila shaka ilishawahi kutokea siku moja mwenza wako akavaa mavazi ambayo hayakukufurahisha, aidha kutokana na ‘urafu’ wake kiasi cha kuweza kuonekana kituko mbele za watu ama alivaa nguo zisizo za heshima zinazoweza kuwafanya watu wakamtafsiri tofauti.

Kama haijawahi kukutokea, binafsi nimeshuhudia wanandoa wakitibuana kwa sababu tu mwanaume amekuwa akimtaka mkewe kubadili staili ya uvaaji wake lakini mke amekuwa aking’ang’ana na mavazi yaleyale ambayo mumewe hayapendi kwa maelezo kuwa, ndiyo aliyozoea kuyavaa.

Kwa wanawake kuna hili suala la kwenda na wakati, kuna mitindo mingi ya nguo imeingia baadhi ikiwa haina matatizo lakini kiukweli kuna mavazi ambayo yamekuwa yakileta mtafaruku mkubwa kwa wanandoa wenye msimamo.

Sikatai kuna uhuru wa mtu kuchagua avae nini akienda wapi lakini kuna mavazi mengine inatakiwa kutumia busara kabla ya kuyaweka mwilini.

Katika hili kabla sijaitumia siku nyingine kuwazungumzia wanaume, nianze na wanawake ambao ndiyo wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutoithamini miili yao na kujikuta wakivaa mavazi yanayoacha wazi sehemu ambazo katika hali ya kawaida zilistahili kuonwa na wapenzi wao tu.

Kuna wanaume wasiopenda kuwaona wake zao wakiwa wamevaa suruali zinazobana na vitopu, vimini na nguo nyingine za kihasara lakini wakati huohuo unakuta mwanamke amezoea kuvaa mavazi hayo tangu alipokuwa mdogo na hakuona tatizo lolote, leo hii ukimwambia asivae mavazi hayo nini kinaweza kutokea?

Naamini mwanamke ataona ananyimwa uhuru wake wa kuchangua na kuhisi ameingia kwenye ndoa na mwanaume ‘anayemaindi vitu vidogo’ lakini je, mke anaweza kuikimbia ndoa eti kwa sababu tu amekatazwa kuvaa suruali wakati yeye amezoea? Ni vigumu na kama atafanya hivyo, huyo atakuwa na matatizo.

Ninachotaka kusema ni kwamba, ndoa inanoga pale ambapo kuna maelewano kati ya wawili waliotokea kupendana. Hivi inapotokea mwenza wako akakueleza kwamba hapendi kukuona umevaa mavazi f’lani kuna ugumu gani kubadilika?

Huoni kwamba kwa kufanya hivyo licha ya kumfurahisha pia ataona unamheshimu na kumsikiliza?

Wanawake wakae wakijua kwamba kinachowafanya wanaume kufi kia hatua ya kuwakataza wao kuvaa aina f’lani ya mavazi katika maeneo f’lani ni wivu na kulinda heshima ndiyo maana naweza kusema kwamba, ukiwa na mtu ambaye hata ukivaa nguo inayoacha wazi matiti na mapaja anachukulia poa tu, huyo hana wivu na wala hakujali.

Achana na ulimbukeni wa kusema eti unakwenda na wakati, waache wale walio nje ya ndoa, wanaojiuza, walioingia katika uhusiano na wanaume wasiojali waendelee kwenda na wakati kwa kuvaa mavazi ambayo hayawezi kuwafanya waheshimike.

Wewe msome mwenza wako na kubaini aina ya mavazi anayopenda kukuona ukiwa umeyavaa. Kuna wanawake wengine hasa wale walio ndani ya ndoa wana tabia ya kuvaa kanga moja tu kisha kukatiza mtaani huku wakitingisha makalio yao tena mbele za wanaume, ili iweje sasa?

Wakutongoze au? Mbona mambo mengine ni kutumia akili tu jamani?

Nihitimishe kwa kusema kwamba, ukiwa chumbani na mumeo vaa upendavyo. Lakini pale unapotoka akikisha unavaa mavazi ambayo hayatamkera.

Ukifanya hivyo kwanza utajijengea heshima lakini pia utamtunzia heshima mumeo na hakika kwa kufanya hivyo utaijengea ndoa yako mazingira ya kudumu. Ushauri wangu ni kwamba, epuka kujifanya unakwenda na wakati katika suala la uvaaji wakati unaiweka rehani ndoa yako.

Niishie hapo kwa leo, kwa ushauri au maoni kama kawaida wasiliana nami kwa namba za simu zilizopo hapo juu.

Kwa maoni na Ushauri: +255 658 798787

Leave A Reply