The House of Favourite Newspapers

UNYAMA: BABA wa SAID Auawa KIKATILI, Kisa Chake Kitakutoa Machozi – VIDEO

INGAWA dhahabu ikipitishwa kwenye moto mara kadhaa huzidi kung’aa, lakini binadamu anapopita kwenye majanga juu ya majanga huhuzunika zaidi; ndivyo ilivyo kwa Said Mrisho anayepita kwenye mikasa mingi mizito, Risasi Jumamosi lina habari kamili.

 

Said ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Aliyetobolewa Macho na Scorpion’ kutokana na kisa cha kusikitisha cha ulemavu wa macho alichokipata miaka mitatu iliyopita, baba yake mlezi, Jisu Ulembo Tuwa ‘70’ mkazi wa Kijiji cha Lukenge, Kibaha, Pwani ameuawa kinyama kwa kuchomwa mkuki ubavuni.

Aliyetobolewa Macho na Scorpion, Said Mrisho

KISA CHA MZEE HUYO KUUAWA NI HIKI

Wanaotuhumiwa kumuua Jisu kwa mujibu wa chanzo chetu ni watu wanaodhaniwa kuwa ni kutoka jamii ya wafugaji ambapo kisa ni mapigano kati yao na wakulima. Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Lukenge Maximilian Mtobu ‘34’ alisema, tukio hilo lilitokea Machi 26, mwaka huu na kusababisha kifo hicho na majeruhi wanne.

 

“Mimi mwenyewe kama unavyoniona nina jeraha usoni, chanzo cha mapigano ni hawa wafugaji kunywesha mifungo yao kwenye visima ambavyo vina maji kwa matumizi ya binadamu. “Kimsingi kama Serikali tulishapiga marufuku ng’ombe kuingizwa kwenye malambo ya maji yanayotumiwa na binadamu lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo.

 

“Hawa wenzetu siku ya tukio waliingiza ng’ombe wao kwenye lambo, mimi na wenzangu tulifika eneo la tukio, nikawa napiga picha ili nitunze kumbukumbu, walipoona hivyo wakanivamia, wakaharibu simu ili wapoteze ushahidi,” alisema.

 

Aliongeza kuwa katika purukushani hiyo kati yao na wafugaji, vijana aliowataja kuwa ni kutoka jamii ya Kimasai walipandwa na hasira na kujikusanya kuzunguka lambo ili kuwazuia wakulima wasiweze kutumia maji hayo.

 

WAKULIMA WARUDI KIJIJINI

“Tulipoona hali inazidi kuwa mbaya tulirejea kijijini kutoa taarifa kwa wenzatu na Kituo cha Polisi Mlandizi.

“Vijana wa jamii ya wafugaji takriban 200 walijikusanya kuzunguka eneo lenye lambo la maji kwa lengo la kuzuia wanakijiji wasitumie maji hayo, jambo lililoamsha hasira kwa jamii ya wakulima ambao nao walijikusanya ili kupambana na wafugaji hao.

“Katika mapigano hayo ndipo ambapo marehemu mzee Jisu akapoteza maisha baada ya kushambuliwa na mkuki na vijana wa jamii ya wafugaji,” alisema Mtobu.

MBUNGE AWAKA

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Abuu Juma alilaani tukio hilo na kuwataka wananchi waendelee kutulia wakati polisi wakifanya uchunguzi na kuwasaka wote waliohusika na vurugu hizo. “Nitoe wito kwa wananchi wote kuepuka vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, niwaahidi kuwa wahusika watasakwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema mbunge huyo.

 

Aidha vikosi vya jeshi la polisi vimeweka kambi katika Kijiji cha Lukenge ili kuimarisha usalama ambapo machafuko yamedhibitiwa. Wakati huohuo mwili wa marehemu Jisu Urembo uliokuwa umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Kibaha ulichukuliwa Machi 27, mwaka huu na ndugu zake na kwenda kuzikwa katika Makaburi ya Lukenge.

 

TUJIKUMBUSHE MACHUNGU YA SAID

Janga la kifo cha Jisu limeamsha upya huzuni kwa Said ambaye mwaka 2016, alitobolewa macho kinyama na mtu anayejulikana kwa jina la Scopion ambaye baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka saba na faini ya shilingi milioni thelathini.

 

Akielezea tukio hilo Said alisema: “Nimesikitika sana baba yangu kuuawa, huyu ndiyo alikuwa kila kitu katika familia kwa maana kwamba hata ndugu zangu alikuwa akiwalea yeye, leo ameondoka na kuniacha katika wakati mgumu.”

Comments are closed.