The House of Favourite Newspapers

Upelelezi Kesi ya ‘Mpemba wa Magufuli’ Wakamilika

SAKATA la kesi ya kukutwa na meno ya tembo inayomkabili mfanyabiashara mwenye asili ya visiwani Zanzibar, Yusuf Ali ‘Mpemba wa Magufuli’, limechukua sura mpya baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hayo yameelezwa leo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba na wakili wa serikali, Florentina Sumawe ambaye alidai kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, Sumawe alieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika lakini jalada la kesi lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kisha litaenda kwa Msajili wa Mahakama Kuu, hivyo kuiomba mahakama iiahirishe hadi siku nyingine.
Hakimu Simba alisema kutokana na hatua hiyo, watasubiri taarifa kutoka kwa Msajili wa Mahakama ili kuwasomea washtakiwa mwenendo wa kesi itakavyoendeshwa mahakama kuu.
Alisema kuwa watafuatilia mahakamani ambapo tena Aprili 18, mwaka huu imepangwa kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo, kama itakuwa tayari watapanga tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo.
Mbali ya Mpemba, washtakiwa wengine ni Charles Mrutu (37), mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40), mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30), mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33), dereva na Pius Kulagwa (46), wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. milioni 785.6.
Aidha, Oktoba 29, mwaka jana walikutwa na vipande 36 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh. milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Na Denis Mtima.

Comments are closed.