The House of Favourite Newspapers

USICHOKIJUA KUHUSU KOFI ANNAN

Kofi Atta Annan

JUMAMOSI iliyopita ya Agosti 18, mwaka huu Afrika na dunia ilipata pigo. Baada ya Nelson Rolihlahla Mandela na waasisi wengine wa bara hili kutangulia mbele ya haki, jabali lingine liliondoka duniani.

MWAFRIKA MWEUSI WA KWANZA

Ni Kofi Atta Annan aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80. Huyu ni Mwafrika mweusi wa kwanza kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN). Akiwa UN, Annan aliongoza kwa mihula miwili, kuanzia mwaka 1996 hadi 2006. Makala haya yawafaa zaidi wanahistoria na wanafunzi ili kuweka historia ya bara hili sawia.

Baada ya UN, Annan ame­kuwa mjumbe maalum wa UN nchini Syria na kuchangia kupa­tikana kwa suluhu ya amani ya mzozo wa nchi hiyo. Mbali na Syria, pia amekuwa msuluhishi wa migogoro ya nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Rwanda, Burundi na Kenya akiwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa. Ni dhahiri ameondoka mwanadiplomasia wa kiwango cha juu kuwahi kutokea.

KOFI ANNAN NI NANI?

Annan alizaliwa Aprili 8, 1938 katika Mji wa Kumasi (wakati huo Gold Coast) nchini Ghana. Alipewa jina la Kofi kuonesha kuwa alizaliwa Ijumaa kuendana na utamaduni wa watu wa Ashanti (Ghana). Jina la Annan linamaanisha kuwa alikuwa ni mtoto wa nne kuzaliwa, alisoma shule za awali na sekondari huko Mfantsipim katika Mji wa Cape Coast, Ghana.

Baadaye alirejea mjini Kumasi na kupata elimu ya sayansi na teknolojia katika chuo ambacho kwa sasa kinajulikana kwa jina la Kwame Nkrumah, Shule ya Sayansi na Teknolojia (jina la mwasisi wa Ghana) kisha alik­wenda kusoma Marekani. Alibobea kwenye uchumi alipojiunga na Chuo Kikuu cha Macalester, Saint Paul, Minne­sota Marekani kisha akabobea kwenye uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Geneva, Uswisi.

Baada ya masomo alihudumu Umoja wa Mataifa kama mchumi mbobezi kabla ya kupanda daraja na kuwa Makamu wa Katibu Mkuu wa UN akihusika na usalama. Alifanya kazi kubwa wakati wa vita huko Rwanda na Yugoslavia na baadaye kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa UN mwaka 1996 hadi 2001.

USICHOKIJUA KUHUSU AN­NAN

Mwaka 1938, alizaliwa huko Kumasi ambao sasa ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ghana.

Mwaka 1962, alianza kufanya kazi Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Mwaka 1965, alimuoa Titi Alakija. Walijaliwa watoto wawili, mvulana na msichana.

Mwaka 1984, alimuoa Nane Lagergren baada ya kutengana na mkewe wa kwanza, Titi.

Mwaka 1991, dada yake ambaye ni pacha wake, Efua alifariki dunia.

Mwaka 1993, alikuwa mkuu wa oparesheni za kulinda amani wa UN.

Mwaka 1997, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa.

Mwaka 2001, alishinda Tuzo ya Amani (Nobel) duniani.

Mwaka 2006, alimaliza muda wa kutumikia UN baada ya kudumu kwa miaka 10.

MAKALA: SIFAEL PAUL NA MTANDAO

Comments are closed.