The House of Favourite Newspapers

Leo Ndiyo Leo, Nani Kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia wa Mwaka 2015?

1

Ballon-DÓr2

Nyota mmoja wa soka kati ya watatu wanaosakata kabumbu katika vilabu viwili vya Hispania Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Neymar leo anatarajia kutajwa kuwa mwanasoka bora wa dunia kwa mwaka 2015.

Nyota huyo atatangazwa majira ya saa 4 na nusu usiku wa leo na kukabidhiwa tuzo ya FIFA ya Ballon d’Or Jijini Zurich Uswisi.

Lionel Messi mwenye tuzo nne za Ballon D’Or hadi sasa, anajivunia rekodi kadhaa alizoweka mwaka 2015 ikiwemo ya kuisaidia klabu yake ya barcelona kutwaa kombe ya Ulaya huku akifunga mabao 10 na kusaidia 6, rekodi ya ufungaji bora wa klabu yake katika mashindano yote ambapo alimaliza msimu akiwa na mabao 43 na kuiwezesha Barcelona kutwaa taji la ligi nchini Hispania pamoja na kombe la Mfalme.

Mbali na kuisaidia Barcelona, pia aliisaidia timu yake ya taifa Argentina kufika fainali ya Copa Amerika.

Cristiano Ronaldo ambaye amekwisha chukua tuzo hiyo mara tatu, baada ya tuzo mwaka jana aliendelea kufanya vizuri hususani katika ufungaji ambapo alimaliza msimu akiwa na mabao 48 huku akilingana na Messi kwa ufungaji katika UEFA Champions League kwa kupachika mabao 10.

Mbali na hilo, katika mwaka huo, Ronaldo alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu ya Real Madrid na kuwapiku Alfredo Di Stefano na Raul.

Mwingine anayewania tuzo hiyo ni Neymar ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona akisaidiana na Messi pamoja na Suarez na kuiwezesha klabu hiyo kutwaa makombe matatu katika msimu mmoja, pamoja na mengine mawili ambayo ni Kombe la dunia kwa vilabu pamoja na UEFA Super Cup yanayoifanya Barcelona kuweka kabatini vikombe vitano ndani ya mwaka mmoja wa kalenda.

Mshindi anapatikana kwa kupigiwa kura na makocha pamoja na manahodha wa timu za taifa huku baadhi ya wadau wa vyombo vya habari pia wakijumuishwa.

1 Comment
  1. Donnie says

    Oooh, nadhani Messi ataichukua tuzo hiyo!

Leave A Reply