The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!-5

0

ILIPOISHIA:
“Amekufa kama ulivyosema.”
“Si nilikwambia? Umeamini sasa!”
“Kwa hiyo wewe ndiyo umemuua? Kwani baba wewe ni mchawi?” nilijikuta nikimuuliza baba swali ambalo hata yeye hakulitegemea, akanitazama kwa macho ya ukali.
SASA ENDELEA…

“Nani aliyekwambia mimi ni mchawi?”
“Nimesikia watu wakisema, hata shuleni kwetu kote watu wananinyooshea vidole wakisema eti mimi na wewe tunashirikiana uchawi,” nilisema huku nikitetemeka, baba akanisogelea kisha akashusha pumzi ndefu.

“Mwanangu Togolai, lazima ujue kwamba hapa kijijini sisi tuna maadui wengi sana kwa sababu ya kazi ninayofanya baba yako. Watu wengi wananionea wivu kwa sababu hakuna mganga mwenye nguvu kama mimi ukanda wote huu. Sasa maadui zangu wameanza kunizushia na kunichafulia sifa nionekane mchawi lakini siyo kweli, mimi ni mganga wala siyo mchawi,” alisema baba kwa sauti iliyojaa busara na upole.

Licha ya maneno yote yaliyokuwa yanazungumzwana watu, nilikuwa nikiamuamini sana baba. Niliyaamini maelezo yote aliyonipa kwa asilimia mia moja, na mimi nikashusha pumzi ndefu kisha tukawa tunatazamana.

“Ikitokea mtu mwingine yeyote anakutania au anakuzodoa kuhusu uchawi, naomba uje unieleze moja kwa moja, wakati mwingine inabidi tuwe wakali ili kulinda heshima yetu,” alisema baba kisha akainuka na kuniacha nimekaa palepale, nikawa naendelea kuyatafakari maneno aliyoniambia.

Japokuwa nilikuwa nampenda sana mwalimu Mwashambwa, sikuweza kuhudhuria kwenye msiba wake nikihofia macho ya watu kwani tayari maneno yalikuwa yamesambaa sana kwamba baba alikuwa anahusika na vifo vya ghafla vya watu wawili, Mwankuga na Mwashambwa vilivyotokea mfululizo.

Hatimaye mazishi yalifanyika lakini manenomaneno yalizidi kuwa mengi kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele. Siku moja nikiwa shuleni, nilisikia wanafunzi wenzangu wakiniteta kwamba mwisho wa ubabe wa familia yetu ulikuwa umefika kwa sababu wanakijiji walikaa kikao cha pamoja na kufikia maazimio ya kwenda kumleta mganga mashuhuri kutoka Chitipa, Malawi kwa ajili ya kuja ‘kuwanyoa’ uchawi watu wote waliokuwa wakihisiwa kuhusika na ushirkina pale kijijini kwetu, akiwemo baba.

“Baba nimesikia eti kuna mganga amefuatwa Malawi kuja kuwanyoa uchawi watu wote wanaotajwa kuhusika kusababisha vifo vya watu wasio na hatia hapa kijijini, ukiwemo wewe,” nilimwambia baba baada ya kurejea kutoka shuleni.

Tofauti na nilivyotegemea, baba hakuonesha kushtushwa na kitu chochote, akawa anaendelea kukatakata mizizi ya dawa nje ya nyumba yetu huku akisema kwamba wanajisumbua kwa sababu yeye siyo mchawi.

“Watanyoana wenyewe kwa wenyewe, mimi hakuna mtu anayeweza kunigusa,” alisema baba kwa kujiamini, nikakosa cha kuendelea kuzungumza. Maisha yaliendelea kusonga mbele, siku saba baadaye, mkutano wa wanakijiji ulitishwa kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Makongorosi ambapo wanakijiji wengi walikusanyika.

“Baba wewe huendi kwenye mkutano?”
“Siendi, kama unataka nenda kaniwakilishe, nina shughuli zangu muhimu siwezi kuziacha kwenda kusikiliza upumbavu wa watu wa kijiji hiki,” alisema baba kwa kujiamini.

Kwa kuwa siku hiyo sikuwa na kazi, ilibidi nifanye kama baba alivyoniambia, nikaenda kumuwakilisha ingawa nililazimika kukaa nyumanyuma, sikutaka watu wajue kwamba niko pale. Niweke wazi kwamba tuhuma zilizokuwa zinamkabili baba na familia yetu kwa jumla zilitufanya tuikose amani kabisa.
Kila tulipokuwa tukionekana, ilikuwa ni lazima tunyooshewe vidole, jambo ambalo binafsi liliniathiri sana kisaikolojia. Nikapoteza kabisa uwezo wa kujiamini, nikawa naishi kama digidigi, hali kadhalika kwa ndugu zangu wengine ingawa kwa baba yeye alionekana kutojali chochote.

“Tumechoshwa na uchawi hapa kijijini kwetu. Kwa pamoja tumefanikisha ujio wa mganga Mabwanji kutoka Malawi kwa lengo la kusafisha kijiji chetu. Wale wote waliokuwa wanaringia uchawi wao, kiboko yao amewasili, karibu uwasalimie wanakijiji,” alisema mzee wa kimila pale kijijini ambaye tulizoea kumuita Mwene.

Itaendelea wiki ijayo…
Kama una mkasa tuma kwa namba hii: 0654 880707

Leave A Reply