The House of Favourite Newspapers

Utaratibu wa pf-3 utazamwe upya

0

image061

NIANZE kwa kutoa pole kwa wananchi wa Kibatini mkoani Tanga kwa kupatwa na msiba mzito, baada ya wapendwa wao nane kuuawa kinyama wiki iliyopita. Licha ya tukio hilo kuwa la kutisha, pia linatoa somo na hadhari kwa vyombo vyetu vya usalama kuwa umakini zaidi unahitajika katika utendaji wa kazi zao.

Leo ningependa kuzungumzia kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa majeruhi yanayotokana na ajali au matukio ya ugomvi, ujambazi na vitu vinavyofanana na hivyo.

Ili majeruhi wa namna hiyo apate kuhudumiwa hospitalini, anapaswa kuwa na fomu maalum ya polisi inayofahamika kama PF-3. Lengo la utaratibu huu, kama ambavyo imekuwa ikizungumzwa mara nyingi ni kuzuia uwezekano wa kumpatia matibabu mtu au watu waliojeruhiwa wakati wakifanya uhalifu.

Ni jambo zuri kuwa na tahadhari hii, lakini kwa kadiri ya mambo yanavyokwenda, ipo haja ya makusudi ya kufanyiwa kwa marekebisho sheria hii, kwani uzoefu unaonesha wengi wanaumizwa nayo.

Mtu amepigwa kisu na kibaka kwa mfano, anakimbizwa hospitalini, lakini hapatiwi huduma bila PF 3. Mwenye hali kama hii, anatakiwa kuhudumiwa haraka kwani jeraha linalotoa damu, lina uwezekano wa kusababisha mauti.

Kuna urasimu mkubwa katika eneo hili, hasa upande wa polisi. Tunapokea malalamiko mengi juu ya watu kuchelewa mno kupatiwa karatasi hizo vituoni, jambo ambalo mara nyingi limesababisha wagonjwa kupoteza maisha.

Ipo haja ya sheria hii kuboreshwa ili kuwalinda wagonjwa. Yatengenezwe mazingira ambayo mtu majeruhi anaweza kupatiwa matibabu wakati taratibu za karatasi hizo zikifanyika, kwani haioneshi busara kwenda kituo cha polisi na mtu anayevuja damu za jeraha la kisu au risasi, badala ya kuwahishwa hospitalini.

Pale vituoni, baadhi ya askari wasio waaminifu, hujichelewesha makusudi kutoa karatasi hizo kwa majeruhi ili kutengeneza mazingira ya rushwa. Baadhi huwatisha watu wenye majeruhi, kwa kuwaambia kuwa mtu wao ni jambazi ilimradi tu watetemeke watoe hongo.

Kama utaratibu utarekebishwa, huenda tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi wasio na hatia ambao hupoteza maisha wakiwa wanahangaikia kupata PF 3 polisi wakati hospitali zipo karibu.

Au kama utaratibu huu ni mgumu, basi angalau kuwe na askari polisi katika hospitali, ili kumsimamia mgonjwa majeruhi ambaye atatiliwa mashaka, wakati matibabu yakiendelea.

Hii ni mojawapo ya sheria zinazopaswa kufanyiwa marekebisho, kwani kukua kwa miji, ongezeko la watu linaloendana na ongezeko la shughuli za kibinadamu, zinafanya vitu vinavyoweza kusababisha majeraha, kuwa zaidi ya uhalifu.

Wakati hayo yakitafutiwa uvumbuzi, nitoe rai kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu kuagiza walio chini yake kuhakikisha majeruhi wanaofikishwa vituoni kwa ajili ya kupatiwa PF 3, wapewe huduma hiyo haraka pasipo kuomba rushwa.

Nachochea tu!

Leave A Reply