The House of Favourite Newspapers

Utata Kijana Aliyefia Mikononi mwa Polisi

ARUSHA: Utata umeibuka kwenye tukio la kifo cha kijana Gerald Mesiyaki (22) mkazi wa Sekei mkoani Arusha anayedaiwa kufariki dunia akiwa ameshikiliwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa kwa tuhuma za ubakaji.

 

Ndugu wa marehemu wamelitupia lawama jeshi la polisi mkoani hapa baada ya kuukuta mwili wa marehemu umefungwa pempas sehemu zake za siri huku akiwa mtupu hana nguo na kwamba wakati anafikishwa kituoni hapo alikuwa mzima wa afya akiwa mevaa nguo zake.

 

Kijana huyo anadaiwa kukamatwa Novemba 9, mwaka huu, saa nane usiku na kundi la wananchi wapatao 10 waliomfuata nyumbani kwa wazazi wake akiwa amelala wakimtuhumu yeye na wenzake watano kuhusika na tukio hilo la ubakaji lililotokea eneo hilo.

Baadaye kijana huyo walimpeleka katika Kituo cha Polisi Sekei kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu.

 

Akizungumza kwa huzuni na Gazeti la Amani, mama mzazi wa marehemu, Ester Mesiyaki na baba wa marehemu Mesiyaki Mungaya, walisema Novemba 9, mwaka huu wakiwa wamelala walisikia kelele za watu nje ya nyumba yao na kutoka ndipo walipomuona kijana wao akiwa amefungwa kamba mikononi na kulazwa chini huku mmoja wa wananchi hao akiwa amemkanyaga mgongoni.

 

Munganya alidai kwamba aliwahoji wananchi hao sababu za kumkamata kijana wake lakini hawakutoa ushirikiano wowote ila aliwatambua baadhi yao akiwemo balozi wa eneo hilo na mwenyekiti wa kitongoji aitwaye Daniel Sambu, hivyo aliamini yupo mikono salama na kuwataka wampeleke kituoni bila kumpiga.

 

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Engolila, Daniel Sambu alikiri kushiriki kumkamata kijana huyo na wenzake wanne na kwamba walikamatwa katika mikono salama na kufikishwa kituo cha polisi bila kupigwa hivyo alishangaa taarifa za kifo cha mtuhumiwa wao.

 

“Gerald alikamatwa usiku na wenzake wanne na wote walifikishwa polisi bila kufinywa, kuhusu kifo cha Gerald ndiyo nasikia kwako ila jambo hilo polisi wanapaswa kulijibu,” alisema Sambu.

 

Kwa upande wa shemeji wa marehemu, Lembris Loshula, alidai kuwa mara baada ya kukamatwa kwa kijana huyo alikuwa akifuatilia tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi ikiwemo kupeleka chakula hadi Jumanne Novemba 12, mwaka huu alipopata taarifa kutoka kwa askari mmoja wa upeleleza (jina linahifadhiwa) kuwa Gerald amefariki dunia.

 

“Taarifa hiyo ilinishitua kiasi cha kutoamini kilichotokea ndipo askari huyo wa upelelezi aliponionyesha picha kupitia simu yake ya mkononi na kumwona marehemu akiwa amelazwa chini kwenye kanga huku akiwa mtupu na sehemu zake za siri zikiwa zimefungwa pempas.

 

“Nilimhoji askari huyo sababu za kifo chake lakini naye aliniuliza iwapo kama marehemu alikuwa na matatizo yoyote ya kiafya; nilimweleza hakuwa na tatizo lolote na siku anachukuliwa alikuwa mzima wa afya,” alisema Lembris.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Johnathan Shana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba marehemu alifikishwa kituoni hapo akiwa na hali mbaya baada ya kushambuliwa na wananchi.

 

“Mtuhumiwa alipelekwa katika Hospitali ya Mount Meru Jumapili Novemba 11 na kulazwa wodi namba sita na baadaye kufikwa na mauti siku hiyo majira ya saa nne asubuhi,” alisema Kamanda Shana.

 

Mwili wamarehemu umehifadhiwa chumba cha maiti katika hospitali hiyo huku ndugu wa marehemu wakigoma kuzika na wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuliingilia kati jambo hilo ili ukweli uweze kujulikana kwani wanaamini ndugu yao hakufa kifo cha kawaida na hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kutokana na kifo hicho.

Makala: Joseph Ngilisho, Amani

Comments are closed.