The House of Favourite Newspapers

MKUU KITENGO CHA USALAMA SHIRIKA LA POSTA ATOWEKA

MKUU wa Kitengo cha Usalama wa Shirika la Posta Tanzania, George Mwamgabe (pichani kushoto), ametoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa muda wa siku nane na hajaonekana ofisini kwake kwa muda mrefu na hakuna taarifa zozote zilizotolewa za kutofika ofisini.

 

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa shirika hilo, Joseph Ngowi, amesema baada ya jitihada za kumtafuta maeneo mbalimbali ikiwamo nyumbani kwake kushindikana, wameona ni busara kutangaza kwenye vyombo vya habari na kwamba wametoa taarifa kuwa anatakiwa kuhudhuria kikao cha nidhamu cha shirika hilo Novemba mosi, mwaka huu.

 

“Ameitwa kwenye kikao cha nidhamu kutokana na kutoonekana kazini na nyumbani, kikao hiki kinataka kumuhoji sababu ya kutoonekana kwake.

 

“Baada ya jitihada za kukutafuta kushindikana kwa kipindi cha zaidi ya wiki moja, tunakufahamisha popote ulipo uhudhurie kikao cha nidhamu kitakachofanyika Novemba mosi majira ya saa 4:00 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano ghorofa ya 12 Posta Makao Makuu kujibu tuhuma za kinidhamu zinazokukabili,” lilisomeka tangazo hilo.

 

Aidha, tangazo hilo limemtaarifu kiongozi huyo kuwa shirika litaendelea na kikao hicho cha nidhamu kama atashindwa kuhudhuria bila taarifa kwa mwajiri wake.

Comments are closed.