The House of Favourite Newspapers

UWOYA ULITAKA NDOA MWENYEWE, TULIA SASA !

Irene Uwoya.

KWAKO muigizaji wa sinema za Kibongo, Irene Uwoya. Habari za siku, mambo yanakwenda vizuri? Bila shaka u-mzima wa afya, nakuona unavyodunda mitaa mbalimbali.  

 

Ukitaka kujua afya yangu, mimi pia sijambo. Namshukuru Mungu mambo yanakwenda ndani ya mjengo wa kufyatua magazeti Pendwa, Global Publishers.

Nimekukumbuka kwa barua leo mama la mama. Nina machache nataka kukueleza maana kwa kweli yananikereketa moyoni na mimi siyo mnafiki, lazima niseme ukweli pale ninapoona hapako sawa.

 

Nimekuwa nikifuatilia siku za hivi karibuni, naliona tatizo kwako katika suala zima la kujiachia kihasarahasara katika mitandao ya kijamii. Sijasema kwamba ni vibaya wewe kuposti katika mitandao hiyo lakini mavazi unayotinga ndiyo yanayonipa mashaka.

Unapiga mavazi ambayo sidhani kama unaweza kukatiza nayo pale mtaa wa Kongo, Kariakoo ukatembea bila kupata usumbufu kutoka kwa vijana wanaouza mitumba. Kifupi ni mavazi fulani ambayo hayana staha sana kwa kuzingatia wewe ni mke wa mtu.

 

Unavaa hivyo ili iweje? Mbona umbo zuri unalo tu, halihitaji hata kuwa nusu utupu ndiyo upendwe.  Bahati mbaya sana, siwezi kusema naingilia kwa undani sana ndoa yenu lakini kwa sababu wewe ni mtu maarufu, acha tu nikuandikie barua. Mavazi yale yanaleta tafsiri mbaya kwako. Watu wanakufikiria vibaya halafu ukiongeza na matanuzi yako, watu wanakosa jibu.

 

Juzijuzi ulikuwa Dubai ikasemekana ulikuwa na mwanaume mwingine, umerudi hujakaa sawa ukatimkia Zanzibar. Misele yote hiyo unaipiga ukiwa peke yako bila mumeo na katika mazingira ambayo yanaleta utata. Nakumbuka pia hivi karibuni, mumeo Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ aliumwa na akalazwa hospitali lakini ilielezwa kuwa hukwenda kumuona.

 

Watu kwenye ukurasa wako wa Instagram walikuona ukitupia picha ukiwa mahali ukila bata zako. Kwa kweli mimi jambo hili naliona si sawa, hivyo unavyofanya utamfanya yule bwana mdogo Janja aishi kwenye mazingira ya mawazo.

Bahati mbaya sana una nyota ya kupendwa na wanaume wako, nakumbuka enzi za uhai wa marehemu mumeo Hamad Ndikumana (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) naye alikupenda sana. Dogo Janja ameshakiri mara nyingi kwamba anakupenda mno, usimpe mawazo basi. Tulia mama.

Ndikumana alipigania penzi lake, hakutamani kukupoteza hata siku moja lakini unajua yaliyotokea hadi Mnyarwanda wa watu akaamua kujiondokea katika mikono yako. Hata hivyo licha ya kuondoka kwako kila tulipokuwa tukimuhoji, aliendelea kusisitiza wewe bado ni mkewe.

 

Ndikumana alionekana kuumia pale ambapo alisikia fununu zozote zinazokuhusisha wewe na mwanaume mwingine. Zilimtesa. Huyu bwana mdogo naye sidhani kama atakuwa anafurahia haya mavazi na hii mitoko yako ambayo mara nyingi inatiliwa shaka.

 

Jiheshimu kama mke wa mtu, usimtese huyu bwana mdogo anaweza kupata ugonjwa wa moyo bure. Kingine, rekebisha uhusiano wako na wazazi wako. Kama hawakubariki hiyo ndoa, una kila sababu ya kutafuta suluhu ili upate baraka zao.

Ni matumaini yangu kwamba ujumbe wangu utakuwa umeuelewa na utaufanyia kazi. Nakutakia mabadiliko mema na asante kwa kusoma barua yangu.

Mimi ni nduguyo;  Erick Evarist.

Comments are closed.