The House of Favourite Newspapers

Vanessa ni funzo kwa mastaa wa kike bongo!

0

Vanessa-Mdee-1.jpgMakala: Hamida Hassan

Staa wa muziki Bongo, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ ni funzo kwa mastaa wa kike Bongo. Nyendo zake tangu aingie kwenye Bongo Fleva hadi akaibuka na tuzo kwenye Kinyang’anyiro cha Afrika Musik Magazine Awards ‘Afrimma’ zilizotolewa Dallas nchini Marekani, wikiendi iliyopita ni kielelezo tosha.

Mara ya kwanza kujulikana alikuwa ni Mtangazaji wa Choice FM ambaye alikuwa akitangaza vema na zaidi alishaini kwenye ushereheshaji wa shughuli ‘MC’.

Nilikutana na Vanessa kwa mara ya kwanza kwenye Mashindano ya Bongo Star Search. Inawezekana nilikuwa nimechelewa kumuona akitangaza jukwaani lakini alikuwa akinikosha kiukweli.

Mara nyingine nilikutana na Vanessa ndani ya Club Bilicanas kwenye Shoo ya MTVBASE ambapo alipanda jukwaani kama mshereheshaji. Nilipomuona nilimtabiria kufika mbali zaidi kutokana na mavazi yake pamoja na utengenezaji wake wa nywele.

Hakika nilikuwa nikimfananisha kama msanii fulani ambaye mbeleni atakuja kujipatia umaarufu mkubwa.

Kumbe sikuwa nimechelewa, baadaye nilimsikia kwenye wimbo wake wa kwanza wa Closer ambao ulimpa sifa kubwa kwenye gemu ikiwa ni baada ya kushiriki kwenye nyimbo mbalimbali kama Monfere na Bashasha wa Bob Junior.

Hata hivyo, Vanessa ambaye kwa sasa anazidi kupasua anga, akaibuka na wimbo wa pili aliotoa uliokwenda kwa jina la Come Over. Hapo ndipo akawa anaachia nyimbo nyingi mfululizo kama Hamjui, Siri na huu wa sasa wa Never Ever. Kwa kigongo hicho, hakika Vanessa amefanikiwa kuliteka soko la muziki kwani ameimba kimataifa zaidi sababu ikiwa ni uimbaji wake na kumudu Lugha ya Kingereza aliyoitumia kwenye wimbo huo.

Ukimwangalia sana, utaona ni binti mdogo kwenye gemu kwani hana siku nyingi sana. Ameanza gemu miaka miwili iliyopita na sasa ana ngoma tano tu za kwake lakini ni tishio kwa mastaa wengine wa kike Bongo kama Sara Kaisi ‘Shaa’, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ , Estalina Sanga ‘Linah,’ Mwasiti Almasi, Khadija Shaban ‘Keisha’, Jokate Mwegelo na wengine.

FUNZO KWA MASTAA WA KIKE BONGO

Anakuwa funzo kwa mastaa wa kike Bongo kwa sababu ni mpiganaji ambaye hapigani kuendelea kuwaimbia Watanzania tu, anapigana kulitangaza taifa zaidi.

Vanessa ameufanya muziki kuwa sehemu ya maisha yake, anajituma sana kuhakikisha anafika mbali.

Wapo wanaodai eti ametokea kwa washua ndiyo maana anapaa haraka lakini mimi nasema ni uthubutu wake tu.

Nasema ni funzo kwa sababu ameweza kuthubutu kuwashinda akina Keisha, Shaa na Mwasiti ambao kwenye hili gemu sasa wanaanza kuzeeka lakini sijasikia wametwaa tuzo, ni kama wameridhika.

SIRI YAKE NI NINI?

Akifunguka mwenyewe anakwambia siri yake ya kufika mbali kimuziki ni kuwekeza akili, nguvu na fedha zake kwenye muziki kwani kwake ni kazi kama ilivyo kazi nyingine.

“Nawasihi mastaa wenzangu wa kike wasichoke, wajaribu kwani kwenye ushindani kunahitaji kuweka nguvu zaidi na mwisho unaibuka mshindi.

“Nawashukuru sana Watanzania kwa kunifanya nikawa juu kwa kunipigia kura lakini mbali na kura zao ni kujituma kwangu kwani hii ni tuzo ya pili kuipata kimataifa,” alisema Vanessa baada ya kutwaa tuzo hiyo ya Afrimma.

Vannesa alipata tuzo ya kwanza ya kimataifa ya All Africa Music Awards ‘AFRIMA’ nchini Nigeria na sasa amepata tuzo ya pili ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki aliyokuwa akiwania na Aster Aweke (Ethiopia), Victoria Kimani (Kenya), Juliana Kanyomozi (Uganda) na STL (Kenya).

Leave A Reply