The House of Favourite Newspapers

VEE MONEY MWANASHERIA ANAYEKIMBIZA KWENYE MUZIKI

 ILE asubuhi wakati ulipoamka unakumbuka kwamba giza lililopita umeota ndoto nzuri inayokufanya utabasamu. Ni ndoto kuhusu mustakabali wa maisha yako ya mbele kwamba umekuwa mtu mkubwa na maarufu duniani kama ambavyo unatamani. Ukiendelea kuelea kwenye furaha na utamu wa mawazo yaliyotawala kwenye akili yako mara unakumbuka juu ya mazingira magumu na changamoto nyingi za kimaisha ambazo unapitia.

Unakumbuka umekwisha zalishwa watoto zaidi ya mmoja na mwanaume amekutelekeza, unakumbuka huna wazazi wala tegemezi wa kukusapoti kufikia ndoto zako, zaidi unaona ugumu wa kufika unakohitaji kwa sababu tu wewe ni mwanamke. Unabaki njia panda, katikati ya kuchagua urudi nyuma usiendelee kupambana kutimiza ndoto zako au usonge mbele kwenye milima na mabonde kuelekea katika safari ya kilele cha kiu ya moyo wako.

Mpenzi msomaji wetu wa Gazeti la Ijumaa, hatuwezi kuchoka kukutia moyo. Tumekwisha kuletea simulizi mbalimbali za maisha ya watu maarufu ambao wamepitia mazingira magumu  kama pengine unayokutana nayo wewe kwa sasa au zaidi wakati wakipigania ndoto zao. Lakini hawakuchoka, walipambana bila kujali ni mazingira gani yanawakabili mpaka wakafika pale walipo kwa sasa.

Nikukumbusha baadhi ya simulizi ni ya mwanamuziki Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ambaye amekuwa mbali na mikono ya wazazi wake, alifanyiwa kitendo kibaya akiwa binti wa miaka 14, akapata mtoto, akaolewa na baadaye kutimuliwa na watoto. Lakini hakukata tamaa, aliamini kupitia kile Mungu alichomjalia ndani yake akapambana na leo ni mtu maarufu na anaishi maisha yake.

Wapo kina Michelle Obama, Oparah Winfrey, Serena Williams, Bona Kaluwa, Fatma Karume na wengine wengi tumewaleta kwako ili uweze kuona namna ‘struggle’ za kutimiza ndoto zinavyohitaji nia ya dhati. Sasa kuhusu siku ya leo, ningependa kukumegea vitu vichache kumhusu mwanadada Vannesa Mdee ‘Vee Money’ ambaye ni mwanamuziki kweye Tasnia ya Muziki wa Bongo Fleva.

NINI VEE MONEY ANAKUFUNDISHA KUHUSU KUTIMIZA NDOTO?

Hili ndilo swali la msingi. Nikwambie tu ukiyatazama maisha ya Vee Money utagundua kwamba ndoto ni kuishi maisha ya kiu ya moyo wako. Vee Money kwa ‘profesheno’ ni mwanasheria wa ngazi ya digrii, aliyochukulia kwenye Chuo cha Catholic University of Eastern Africa, kilichopo Kenya.

Lakini jifikirie kuhusu hili. Vee, aliweza kuachana na taaluma yake hiyo, akaamua kufuata ndoto zake. Ambapo alianza na utangazaji lakini yote hiyo alikuwa anatafuta njia kuingia kwenye muziki ambao ndiyo kila kitu kwenye maisha yake. Hii ndiyo maana ya ndoto. Hata kama umebahatika kuwa mtu gani, ni vigumu kuwa na furaha usipobahatika kuishi au kufanya yale unayotamani ni vigumu kupata furaha kwenye maisha yako.

KABEBA TUZO NYINGI

Kwa upande wa wanamuziki wanawake kwa Bongo, ndiye mwanamuziki anayeshikilia rekodi kwa kuchukua tuzo nyingi ndani miaka michache. Vee Money toka mwaka 2013 mpaka sasa (ndani ya miaka mitano), amefanikiwa kubeba tuzo mbalimbali zipatazo 11 na sasa anawania Tuzo ya Afrimma 2018. Tunaweza kusema huyu ndiye Lady Jaydee wa kizazi cha sasa na pengine akikazana anaweza kufikia rekodi yake ya tuzo 38, kwa miaka 15!

NI MSAADA MKUBWA KWA JAMII

Mwandishi Robin Sharma wa kitabu cha The Monk Who Sold His Ferrari, aliandika kwenye kitabu chake hicho kwamba hakuna kitu kizuri ambacho unaweza kujifanyia mwenyewe kama kuwekeza muda kwa ajili ya kuboresha uwezo wako wa kufikiri, uwezo wa kufanya kazi na kupambana kuelekea kwenye ndoto zako. Lakini pia aliongeza; unapokuwa na ndoto unatakiwa kujiuliza je, kupitia ndoto zako unaweza kuwasaidia wengine? (jamii.)

Kwa Vee Money, ndoto zake mbali na kumsaidia mwenyewe ni msaada mkubwa pia kwa jamii. Mara kwa mara amekuwa akitoa msaada kwenye vituo mbalimbali vya watoto wahitaji na miezi ya hivi karibuni amekuwa akisaidia shule mbalimbali Arusha ambazo hazina mazingira mazuri na zinahitaji msaada. Unaweza kuchangua pia njia yako kama Vee Money, ishi maisha yako!

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.