The House of Favourite Newspapers

Video: Aeleza Alivyofungwa Miaka 26 Gerezani kwa Wizi wa Saa ya Sh 200 (Part 01 & 02)

HUNA sababu ya kujilaumu na kukata tamaa kwa sababu tu, unaamini unapitia kipindi kigumu sana katika maisha yako, kuna wengi wamepitia na hawakurudi nyuma wala kukata tamaa.

Ingawa upande wa pili natamani kama ungepata nafasi ya kuweza kusikia na kuona matatizo ya watu wengine, bila shaka ungejifunza kwamba, hustahili kukata tamaa.

Mmoja wa watu ambao wana mikasa ya maisha yao, yenye uchungu na kupoteza muda mwingi pasipo kutegemea ni Severine Faustine (55). Yeye ni mkazi wa Bagamoyo mkoani Pwani ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 40 kwa kosa la kumnyang’anya saa na kumjeruhi mkono rafiki yake.

Faustine hakujua kama angefungwa miaka hiyo yote lakini pia hakujua kama kitendo cha kumpora saa rafiki yake kingempeleka polisi kisha gerezani miaka 40 ambayo ni umri wa mtu kuanzia kuzaliwa, kusoma, kuoa wakati mwingine mpaka kufa au kuwa kiongozi wa nchi.

saa

Mwenyewe anasema hajui nini kilitokea lakini kwa sehemu kubwa anaamini ni ujana. Aliingia jela akiwa na miaka 28 tu (ujana mbichi) na ametoka Oktoba 27, mwaka 2016 akiwa na miaka 55. Hebu vuta picha msomaji. Ungekuwa wewe baada ya kutoka ungefanya nini? Unaingia kijana, unatoka ukiwa unanusa uzee.

Achilia mbali na hakimu kumkuta na hatia, lakini ukweli unabaki palepale kwamba, inauma sana.

 

TWENDE NAYE PAMOJA:

Mimi naitwa Severine Faustine, nilizaliwa mwaka 1961 Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Natoka katika kabila la Wamakonde nikiwa ni mtoto wa kwanza kuzaliwa kwenye familia yenye watoto 11.

Mwaka 1971 nikiwa na miaka 10, nilianza masomo yangu ya awali katika Shule ya Msingi Mwambao iliyopo Bagamoyo na nilifanikiwa kumaliza mwaka 1977.

Sikufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari au kidato cha kwanza kama inavyojulikana na wengi kutokana na mazingira duni ya nyumbani kwetu lakini pia hata familia yenyewe haikuwa na mwamko wa elimu, kwani  kwa wakati ule, mimi ndiye angalau nilikuwa miongoni mwa waliofanikiwa kumaliza darasa la saba kwenye familia, labda kama ndugu zangu walijiendeleza kipindi mimi nikiwa gerezani.

 

AMALIZA DARASA LA SABA, AANZA KUSAKA PESA

Kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari niliamua kujiingiza kwenye shughuli mbalimbali ili niweze kujipatia kipato kwa maana ya fedha kwa kufanya kazi ya ujenzi na biashara ndogondogo palepale Bagamoyo.

 

ATIMKIA KIBAHA

Lakini baada ya kuona maisha hayaendi vizuri pale Bagamoyo niliamua kuhamia kwa babu yangu, mzee  Fredinando Kandinya aliyekuwa anaishi Kibaha Kwamfipa. Babu alinipokea, nikaanza shughuli ndogondogo ikiwemo kuuza sigara na nyinginezo ambazo niliamini zingeweza kusaidia kuniingizia kipato kwenye mifuko yangu.

Kama ilivyo kawaida ya vijana mnapokuwa wengi ni lazima mtakuwa na maskani yenu (kijiwe) kwa ajili ya kukutania na kupiga stori za hapa na pale ili kupoteza muda.

Miongoni mwa vijana waliokuwepo maskani pale ni jirani na rafiki yangu mmoja ambaye tulimzoea kwa jina la President (Rais). Huyu President kwangu mimi alikuwa kama mdogo wangu, kwani nilimzidi umri kidogo lakini pia alikuwa kama ndugu kutokana na ujirani, wazazi wake wanilijua.

 

KISA CHA KUFUNGWA KILIANZIA HAPA

Sasa, maisha ya pale maskani yalikuwa ya kubangaizabangaiza. Lakini pamoja na hali hiyo na kukaa maskani muda mwingi na vijana wenzangu, mimi sikuwa natumia kilevi chochote. Yaani sikuwa navuta  bangi, unga (madawa ya kulevya), pombe, sigara na vinginevyo.

Sasa siku moja, tukiwa pale maskani, mimi nilimfanyia utani President. Nilimpokonya saa yake ya mkononi. Kama nilivyosema, nilifanya vile kama utani, kwani tulizoea kutaniana. Na mimi ni mtu wa kupenda utani sana.

Sasa baada ya kumpokonya ile saa, President  alinifuata na kutaka kuichukua kwa nguvu mimi ‘nikampushi’, akadondoka chini hali iliyomsababishia achubuke sehemu ya kiwiko cha mkono.

Niliondoka pale maskani. Lakini kama nilivyosema, nikijua ni utani na mimi dhamira yangu haikuwa kumpora bali kuchukua na kuivaa kisha kesho yake nimrejeshee kwani ni watu ambao tupo pamoja kila siku ya Mungu.

 

AFIKISHWA KITUO CHA POLISI

Nyuma yangu, kumbe President aliondoka kwa hasira pale maskani na kwenda Kituo cha Polisi Kibaha kunishitaki kuwa, nilimpora saa na kumjeruhi. Kiukweli sikuwa na nia ya kumpokonya kwani ni mtu ambaye tulikuwa tukishinda naye maskani ni rafiki na jirani yangu, sema mambo mengine ni ujana tu ndiyo ulikuwa unasumbua kwa wakati ule.

Ndugu zangu pamoja na wazazi wake kumkalisha kitako President na kumsihi kulimaliza suala lile kifamilia lakini jamaa hakukubali kabisa.

Kwa hiyo nilichukuliwa na kupelekwa polisi. Hapo ilikuwa Novemba 11, mwaka 1989  nikiwa na umri wa miaka 28 tu. Nilikaa mahabusu hadi Januari 2, 1990 nikapelekwa mahakamani palepale Kibaha.

Dah! Kusema ukweli kama binadamu tungekuwa tunajua lolote la kesho, kuna mambo tungekuwa tunajiepusha nayo mapema sana. Lakini pia nilikubaliana na msemo wa wahenga kuwa, rafiki yako wa leo anaweza kuwa adui yako wa kesho na adui yako wa kesho akawa rafiki yako wa keshokutwa. Hiyo inawezekana kabisa.

Mimi sikutegemea kama President angeweza kunifikisha polisi kwa utani ule. Mbaya zaidi ni kwamba, familia zote mbili, kwa wazazi wake na kwa babu yangu, zilimuomba tukae chini ili kuyamaliza kindugu lakini jamaa alikataa katakata.

 

Je, unajua nini kiliendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo…

Comments are closed.