The House of Favourite Newspapers

Video: Msanii Idris Sultan Afikishwa Mahakamani Dar

0
Mchekeshaji, Idris Sultan.

MSANII wa vichekesho nchini, Idris Sultan (27) na wenzake wawili leo Machi 20, 2020, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kujibu shtaka  la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

 

Mbali na Sultan, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Doctor Ulimwengu (28) mkazi wa Mbezi Beach na Isihaka Mwinyimvua (22) ambaye ni msanii na mkazi wa Gongo la Mboto.

Washtakiwa hao wamesomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Mushi alidai washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 60/2020.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8, 2016 na Machi 13, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa kutumia Online Tv inayojulikana kwa jina la Loko Motion, walichapisha maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka TCRA, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

 

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

 

Hakimu Shaidi, alitoa masharti ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh 8milioni.

 

Pia, mdhamini huyo anatakiwa kuwa na barua inayotambulika kisheria na kitambulisho cha Taifa.

Washtakiwa wote wametimiza masharti ya dhamana na hakimu Shaidi, ameahirisha kesi hiyo hadi April 21, 2020 itakapotajwa.

Leave A Reply