The House of Favourite Newspapers

Vigogo Madawa ya Kulevya Wanaswa na ‘Unga’ Kilo 270 – Video

0

MAMLAKA ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya juzi Aprili 15, 2020, imefanikiwa kumkamata kigogo wa dawa za kulevya raia wa Nigeria, Kanayo David Chukwu (39),  mkazi wa Masaki jijini Dar es Salaam.

 

Pia inawashikilia raia wawili wa Tanzania, Alistair Amon Mbele (38) ambaye ni Mkutubi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan jijini Dar es Salaam, mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa na Isso Romward Lupembe (49) ambaye ni mkazi wa Mbezi Louis na Changanyikeni jijini.

 

Watuhumiwa wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya heroin zinazokadiriwa kuwa na zaidi ya kilogramu 270 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye moja ya nyumba iliyopo Mbezi Kibanda cha Mkaa.

 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, James Kaji,  amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa muda mrefu nchini na kwamba mamlaka imefanikiwa kukamatwa kutokana na jitihadana  ushirikiano uliopo kati ya nchi yetu na nchi nyingine katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya duniani kutokana na utaratibu wa kubadilishana taarifa ambazo husaidia kurahisssha ukamataji huo.

 

“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa vyombo mbalimbali vya usalama ndani na nje ya nchi tulianza kuwafuatilia toka tarehe nane na kufanikiwa kuwaweka mtegoni tangu wakiwa wanateremsha mzigo na kufanikiwa kuwakamata.

 

“Pia watuhumiwa hao walikuwa wamefanya maandalizi ya kupokea mzigo huo kwa kujenga tenki la maji machafu ambalo liliwekwa chemba juu ya kuhifadhia dawa hizo na bahati mbaya mzigio uliwahi kufika kabla tenki halijakamilika, hivyo kulazimika kuzihifadhi ndani ya nyumba,”amesema Kamishna Kaji.

 

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa ajili ya kuokoa maisha ya Watanzania kwa kutoa taarifa pale wanapoona matukio yasiyo ya kawaida kwa usalama.

 

“Kilo hizi ni nyingi sana zingeingia mtaani zingeathiri nguvu kazi ya vijana wetu huko mitaani kwa kiasi kikubwa. Ninasikitika kuona bado kuna watu wasio na utu, wanaendelea kujitafutia kipato kwa njia hii haramu bila kujali. Ninatoa rai kwa Watanzania walio tayari kuwapambania watoto wao kuendelea kushirikiana na mamlaka kuwafichua watu hawa bila woga,” amefafanua.

 

Ameongeza kuwa watuhumiwa wako mikononi mwa mamlaka na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika ili sheria ichukue mkondo wake.

 

Leave A Reply