The House of Favourite Newspapers

VIKOBA VYAZUA BALAA DAR !

KIKUNDI cha Vicoba cha Upendo chenye masikani yake huko Kibugumo-Kigamboni jijini Dar kimejikuta katika sintofahamu kufuatia mweka hazina wake aliyefahamika kwa jina la Mwasiti Bakari kutoweka na kuzua balaa kubwa.  

 

Wakizungumza na Amani hivi karibuni, baadhi ya wanachama wa kikundi hicho waliokuwa wamefura kwa hasira walisema kuwa, wamenusa harufu ya ufisadi kwenye pesa zao hivyo wameamua kumfungia kazi Mwasiti ili waweze kupata haki zao.

 

Walisema walianza kutoa michango yao kwa kipindi cha mwaka mzima hadi wakafikisha kiasi cha shilingi milioni 8 lakini kwa walipofikia wanaona dalili ya pesa hizo kuyeyuka. Fatuma Robert ambaye ni mmoja wa wanachama wa kikundi hicho ameliambia Amani kuwa, walianzisha kikundi hicho kwa lengo la kujikwamua kiuchumi lakini sasa wanajuta.

“Sisi tulianzisha kikundi chetu mwaka jana mwezi wa pili, tulichagua viongozi akiwemo mwenyekiti, katibu na mweka hazina. Tukawa tunaweka hela sasa mwaka umeisha tukaambiwa kuwa inatakiwa tugawane mwezi wa pili ili tuanze upya lakini tunaona tunapigwa kalenda tu.

 

“Tukakubaliana kama kikundi tumfuate mweka hazina nyumbani kwake ili tuweze kujua nini kinaendelea. Tumefika pale tumemkuta mumewe, yeye hayupo na ameondoka na watoto.

“Tumejaribu kumtafuta kupitia simu yake ya mkononi hapatikani. Mazingira hayo yanatufanya tuhisi tumepigwa ila sisi tunamuomba huko aliko ajue kwamba tunataka haki yetu na haiwezi kupotea kirahisi. Ni bora ajisalimishe tu,” alisema Fatuma.

 

Naye Kulwa Ng’azi alisema: “Kila tulipokuwa tunakutana mweka hazina alikuwa anatuhamasisha sana kuweka hela, tukawa tunajinyima kula vizuri, watoto wetu wanakula maharage kila siku tukitarajia mwisho wa mwaka tutapata hela yetu.

 

“Lakini mpaka sasa mweka hazina hajulikani yupo wapi, cha ajabu mume wake wanawasiliana na analeta hela kwa mwenyekiti Mwajuma Halidi kwa ajili ya marejesho ya mkopo mwingine, kwa nini asije kutupa pesa zetu? Hata kama tutapata kidogokidogo ni jasho letu.”

 

Imezidi kuelezwa kuwa, kufuatia kuingia mitini kwa mweka hazina huyo, wanakikundi hao walilazimika kwenda kuripoti polisi na kufungua jalada la kesi lenye namba KGD/RB/1457/2019 WIZI WA KUAMINIWA. Naye mwenyekiti wa kikundi hicho, Mwajuma Halidi alisema anamuomba mweka hazina huyo popote alipo arudishe hela za wanachama kwa kuwa wana mambo ya msingi ya kuzifanyia.

“Nakuomba Mwasiti popote ulipo urudi ili uwape hela zao wanachama nikiwemo mimi, hela kwa sasa ni ngumu kuipata na tunashindwa kufanya mambo ya muhimu, wakati tunachanga pesa tulitarajia kuja kunufaika baadaye lakini leo hii tunateseka,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza:

 

“Mpaka sasa wanachama wanajua mimi na mweka hazina letu moja, kwamba nimeshirikiana naye kula hela. Mimi sijala hela, yeye arudi tu ili aje kutulipa hela zetu.”

 

Kufuatia tukio hilo, mmoja wa wanachama hao alitoa tahadhari kwa wengine waliojiunga na Vicoba kuwa makini na watu wanaowachagua kuwaongoza kwani wasipoangalia yanaweza kuwakuta kama yaliyowakuta wao.

 

“Sisi yametufika, niwatahadharishe tu wengine walio kwenye Vicoba kuwa makini maana kuna watu wengine wakipewa dhamana ya kushika pesa, tamaa zinawaingia, jambo ambalo ni baya sana,” alisema Jamila Hamis.

Comments are closed.