The House of Favourite Newspapers

Vutuo Vipya vya Afya, Zahanati Kuanza Kutoa Huduma Januari 29, 2024

0

Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ameziagiza Timu za Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri (RHMT na CHMT) nchini kuhakikisha kuwa Vituo vya Afya na Zahanati ambavyo ujenzi wake umekamilika vianze kutoa huduma za awali kwa wananchi wa maeneo husika kuanzia Januari 29 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Dkt. Mfaume wakati akizungumza na Watumishi wa Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri Mkoani Morogoro wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya kukagua na kuangalia ubora wa huduma za Afya Mkoani humo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa Serikali imetoa fedha za ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya hapa nchini ambapo kwa asilimia kubwa ujenzi huo umekamilika lakini huduma hazijaanza kutolewa hivyo wamezitaka Timu hizo kuhakikisha huduma za awali zikiwemo za OPD, upimaji, huduma za mama na mtoto na upasuaji zianze kutolewa ifikapo Januari 29 mwaka huu.

“…naagiza na haya ni maagizo yangu kwa CHMT na RHMT nchi nzima zile huduma za awali ambazo majengo yake yamekamilika zianze kutolewa Januari 29…amesema Dkt. Mfaume.

Aidha, amezitaka timu hizo kusimamia Vifaa tiba vinavyopelekwa katika vituo vyao na kuhakikisha kuwa vinatunzwa na kutumika kama ilivyokusudiwa huku akiwataka kujiepusha na wizi wa vifaa hivyo na kwamba Serikali haitamfumbia macho mtumishi yeyote atakayebainika kufanya ubadhirifu wa vifaa tiba.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mfaume amewataka Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo yao hususan kipindi hiki cha mvua nyingi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa ziara yake huku akimuhakikishia kuwa maoni, maelekezo na maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake na wakati wa majumuisho watayafanyia kazi ili huduma za Afya Mkoani humo ziimarike.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Mziha akiwemo Bi. Angela Chengula ameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea kituo cha Afya ambacho kimejengwa kupitia fedha za Tozo za miamala ya simu Shilingi milioni 500 na kwamba kituo hicho kinaenda kuwaondolea adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 60 kufuata huduma za Afya.

Mkurugenzi huyo wa Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii amefanya ziara ya siku tatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mvomero na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo alikagua ujenzi wa Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.

Leave A Reply