The House of Favourite Newspapers

Vyuma Vitatu Vimebaki Simba Kufunga Usajili Msimu wa 2023/24

0
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally

UONGOZI wa Simba, umeibuka na kutamka kuwa, umebakisha wachezaji watatu pekee kwa ajili ya kufunga usajili wao wa msimu wa 2023/24.

Simba hadi hivi sasa imekamilisha usajili wa wachezaji watatu na kuwatambulisha ambapo walianza na kiungo mshambuliaji Mcameroon, Willy Onana kutoka Rayon Sports ya Rwanda, kisha kiungo Aubin Kramo aliyetokea ASEC Mimosas na juzi ilikuwa zamu ya beki wa kati kutoka Cotton Sports ya Cameroon, Fondoh Che Malone.

Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema wanaofikiri wamemaliza usajili, basi wanajidanganya kwani bado kuna wachezaji wengine watatu waliokamilisha usajili wao, wakisubiri kutambulishwa.

Ally alisema wachezaji hao watakaotambulishwa ni hatari na tishio ambao wanakwenda kuipeleka Simba hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kutwaa taji la Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports msimu ujao.

Aliongeza kuwa, wachezaji hao watatambulishwa kuanzia leo Jumanne mara baada ya taratibu za usajili kukamilika.

“Kwa wale wanaofikiri sisi Simba tumemaliza usajili, basi niwaambie bado tunaendelea na usajili mkubwa wa wachezaji wa viwango vikubwa Afrika watakaoipa mafanikio timu yetu.

“Ndani ya wiki hii usajili huu utakuwa umekamilika sambamba na kuwatambulisha wachezaji wetu wapya waliokuwepo katika mipango yetu ya msimu ujao unakwenda kuwa wa kihistoria.

“Utambulisho utafanyika ili kupisha benchi la ufundi kuanza ‘Pre Seasson’, hivyo ndani ya wiki hii kila kitu kitakamilika,” alisema Ally.

Leave A Reply