Wabunge Marekani Wataruhusiwa Kuvaa Wanavyotaka Wakiwa Bungeni
Kuanzia Jumatatu ya jana wabunge nchini Marekani wataruhusiwa kuvaa vile wanavyotaka wakiwa Bungeni.
Akizungumza na Shirika la habari la CBS Kiongozi wa Wabunge wenye uwakilishi mkubwa Seneta Chuck Schumer amesema kuwa “Wabunge watavaa wanavyotaka lakini mimi nitaendelea kuvaa suti”
Aidha wafanyakazi wengine wote wa Bunge watatakiwa kuendelea na kanuni ya mavazi ya kiofisi kama ilivyo kawaida.
Uamuzi huu ambao sio sheria utampa wepesi zaidi seneta John Fetterman ambaye tangu mwezi Aprili aliporudi kutoka kwenye likizo ya matibabu amekuwa akivaa anavyotaka.
Kutokana na mavazi yake kuna nyakati ilimlazimu Fetterman kukaa tofauti na wengine pia kutumia ishara za vidole kupiga kura Bungeni humo ili kutouvunja utaratibu wa kanuni za mavazi.
Nao upande wa upinzani umeukosoa uamuzi huo na kusema kuwa unalishushia heshima Bunge na kuubadili utaratibu wa kihistoria wa kuvaa suti bungeni.
” Kanuni za mavazi ni moja ya mambo yanayoweka viwango, adabu na heshima katika mashirika” alisema muwakilishi mmoja wa wapinzani.