Wakamatwa kwa kula mfungo wa Ramadhani

 

POLISI wa Sharia ya Kiislamu katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la The Islamic Sharia Kano wamewakamata kwa muda watu 80 walioshukiwa kwa kula hadharani badala ya kufunga kuanzia alfajiri hadi jua linapotua kulingana na maagizo ya dini ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 

Polisi wa Sharia wanaofahamika kama Hisbah, wamesema kuwa watu hao walikamatwa  nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kano katika kipindi cha siku kadhaa.

 

Jimbo la Kano ni moja ya majimbo kadhaa ya kaskazini mwa Nigeria ambako Sharia ya Kiislamu ilianzishwa upya tangu mwaka 2000.

 

 

Sharia ya Kiislamu inatekelezwa sambamba na sheria ya kawaida kwenye majimbo hayo. Msemaji wa Hisbah katika jimbo la Kano, Adamu Yahaya, ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa wote waliokamatwa walikuwa ni Waislamu na maofisa hawawalengi wasio Waislamu kwa sababu hawafungwi na sheria ya Kiislamu.

 

Amesema kuwa baadhi ya wale waliokamatwa waliiambia ofisi ya Sharia kuwa walikuwa wanakula kwa sababu hawakuuona binafsi mwezi wa Ramadhani huku wengine wakisema walikuwa ni wagonjwa, lakini maofisa walisema kuwa madai yao hayakuwa na msingi wowote.

 

Watu hao 80 walionywa na kuachiliwa huru kwa sababu walikuwa wamefanya kosa hilo kwa ”mara ya kwanza” alisema Bwana Yahaya.

 

Walionywa kuwa iwapo watakamatwa tena, watapelekwa mahakamani. Hisbah wamesema kuwa wataendelea kufanya doria katika kipindi chote cha Ramadhani kwa lengo la kuwakamata Waislamu wote ambao hawafungi katika mwezi huu.

 

Mfungo wa Ramadhani ni lazima kwa kila mtu mzima Muislamu, lakini baadhi ya watu kama vile wenye magonjwa makubwa, hawatakiwi kufunga.

Loading...

Toa comment