WAKAZI wa Kata ya Somangila wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam wamemuomba Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuingilia kati suala la mgogoro uliopo kwenye kata hiyo uliokwamisha miundombinu ya barabara.
Hayo yamebainishwa na wakazi wa eneo hilo wakati wakizungumza na waandishi wa habari walipokuwa wamekutana na Diwani wa Kata hiyo, Chichi Masanja na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo, Sadick Mohamed, ambapo wameelezea kuhusu kero yao ya miundombinu ya barabara ambayo imekwamishwa na mmoja wa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa mmoja hapa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao wameelezea kwamba mkurugenzi huyo (wakamtaja ) amezungushia uzio kwenye eneo la barabara, hivyo kusababisha usumbufu hasa kwa akina mama wajawazito wanapohitaji kwenda kujifungua.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo kijiji cha Dege Kata ya Somangila, Sadick Mohamed, amesema kuwa mkurugenzi huyo amejimilikisha zaidi ya ekari 100 ambazo haziendelezwi na hivyo zimesababisha kuwepo kwa wahalifu wanaojificha kwenye vichaka vilivyopo kwenye mashamba hayo.
Amesema kuwa mbali na wahalifu pia amekwamisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara unaosimamiwa na TARURA ambayo tayari fedha zake zilikwishatengwa katika bajeti ya 2017/18 hivyo ujenzi huo ukiendelea kusimama fedha hizo zinaweza kurudi serikali kuu.
Wakati huohuo, Masanja amesema ni vyema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aingilie kati suala hilo kwani linakwamisha maendeleo katika wilaya hiyo.
Comments are closed.