The House of Favourite Newspapers

Waliosababisha Ndege Kukamatwa Sauz Kushitakiwa – Video

MSEMAJI Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbas amesema watakaobainika walifanya hujuma dhidi ya  serikali  na kusababisha kuzuiwa kwa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) nchini Afrika Kusini watafunguliwa kesi ya kuihujumu nchi baada ya kumalizika kwa kesi ya kuzuiwa kwa ndege katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini.

 

Akizungumza mjini Dodoma leo Jumamosi Agosti 31, 2019,  Dkt.  Abbas amesema wapo Watanzania wanaoshiriki kuihujumu serikali  kuhusu ndege hiyo, wakifikiri kwamba kuna siku uhujumu huo utawasaidia.

 

“Wapo wazawa wanaofanya mawili, matatu kuhujumu nchi lakini niwaeleze tusubiri kesi iishe huko Afrika Kusini, tutawafungulia kesi ya kuhujumu nchi yetu.

 

“Hakuna nabii katika historia ya manabii aliyewahi kuaminiwa kwa asilimia 100, hivyo huwezi kukubaliwa na watu wote, hata hii ndege inayoshikiliwa ikija Tanzania ipo siku wanaochukia watatumia usafiri huo kwenda Afrika Kusini kama sio wao basi watoto wao,” amesema.

 

 

Jana, mawakili wa Tanzania katika kesi  hiyo waliitaka Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kutupilia mbali zuio la kuzuia ndege ya shirika hilo aina ya Airbus A220-300, wakisema ilitolewa kimakosa.

 

Ameendelea…

 “Nawapongeza ndugu zangu waandishi wa habari kwa kazi nzuri ya kutoa taarifa kwa wananchi wakati wa kipindi chote cha mkutano wa SADC. Tanzania itakuwa mwenyeji wa Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki (JAMAFEST) kuanzia tarehe 21-28 Septemba, 2019, ambapo litahusisha takribani watu 100,000 kutoka nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

 

“Taasisi zetu zimeendelea kunufaika na SADC, ikiwa hivi karibuni Bohari ya Dawa (MSD) imekamilisha mfumo wa kusambaza dawa nchi za SADC, TTCL inaendelea kusambaza Mkongo wa Mawasiliano katika nchi za Zambia na Malawi. Heshima ya Tanzania imeendelea kupanda kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Dkt. John Magufuli.

 

“Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Julai 12, 2019, kwa pamoja kati ya Transparency International na Afro-Barometer, Tanzania imeongoza katika nchi 35 kwa juhudi za wazi katika kupambana na rushwa. Jumla ya Tsh Bil. 25.5 zimerejeshwa Serikalini, ikiwa ni pamoja na Tsh Bil. 14.6 za urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu, na Tsh Bil. 10.9 za thamani ya mali zilizotaifishwa ikiwamo magari manane, vituo vya mafuta na nyumba.

 

“Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani Tsh Bil. 46.9 kutokana na kutofuatwa kwa taratibu za ununuzi, malipo zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana.

 

“Julai 2019 nchi yetu ilipata fursa ya kipekee ya kumulikwa na JARIDA LA FORBES AFRIKA katika toleo lililokuwa na kichwa cha Habari “TANZANIA-BUILDING PROSPERITY” likimtaja Rais Magufuli kuwa kiongozi mwenye maono makubwa.

 

“TUMEAMUA kuanza safari ya miaka mitatu ya Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere utakaozalisha megawati 2115, ikiwa ni mradi wa nne mkubwa wa kufua umeme Afrika, utakaogharimu Tsh. Tril 6.5,  ambapo mpaka sasa Serikali imeshatoa Tsh Tril. 1.07.

 

“Serikali inaendelea kukamilisha Mradi wa Upanuzi wa Kinyerezi -1 ambao kwa sasa umefikia zaidi ya 90%. Mradi huo wa megawati 185 utakamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, ambapo gharama za mradi huo ni Dola za Marekani mil. 188 na Serikali imeshalipa Dola mil. 128.”

Comments are closed.