The House of Favourite Newspapers

Waliotishia Kuuawa ‘Wakutana’ na RC

0

MKUU wa Mkoa wa Pwani; Mhandisi Evarist Ndikilo, amekutana na wafugaji ambao baadhi yao wamewatishia kuwaua wakulima ambao wamemlalamikia kiongozi huyo kuwa, wanatishiwa kuuawa baada ya mazao yao kuliwa na mifugo wilayani Chalinze, mkoani humo.

 

Kutokana na kukutana na kero hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhandisi Ndikilo aliwapa polisi wilayani Chalinze siku tatu kuhakikisha wamewakamata wafugaji wawili wakazi wa Msata kutokana na tuhuma hizo za kutishia kuwaua wananchi baada ya kulisha mifugo yao katika bustani ya wakulima.

 

Amri hiyo aliitoa baada ya watuhumiwa kutajwa kuwa ni Demisi Kichele na Julius Nyangura ambao kwa pamoja, wanadaiwa kumtishia kumuua mkulima Selemani Salum, licha ya kulisha mifugo yao katika bustani yake.

Aidha, watendaji wa kata, vitongoji na vijiji vya Msata, wamepewa mwezi mmoja na mkuu huyo wa mkoa kujitathmini.

 

Mhandisi Ndikilo ametoa maagizo hayo, alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza kero za wananchi katika kata hiyo.

Akiwa Msata, Mhandisi Ndikilo alielezwa kwamba, baadhi ya wafugaji katika eneo hilo, wamekuwa wakiwanyanyasa wakulima na kutamba kwamba, wameiweka mifukoni serikali kijijini hapo.

 

“Naagiza, viongozi hakikisheni wafugaji hao wanalipa fidia ya shilingi milioni moja kwa mkulima (Selemani Salum) mwenye bustani baada ya kulisha mifugo yao kwenye bustani hiyo ya robo eka iliyokuwa imelimwa nyanya na mbogamboga mbalimbali,” alisema Mhandisi Ndikilo.

 

Alionya kuwa, endapo agizo lake hilo halitatekelezwa, atawasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro kumweleza tabia ya baadhi ya polisi ambao huwapa nguvu na kuwalinda wafugaji wenye makosa.

 

“Haiwezekani polisi imuombe mkulima awasamehe wafugaji kutolipa fidia wakati wamepata hasara, jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kutenda haki na kulinda amani. Ni lazima kuanzia sasa, polisi mtende haki bila upendeleo,” alionya.

 

Akizungumzia bonde la Mto Ruvu, Mhandisi Ndikilo alisema, kila mtu ana haki ya kulitumia pasipo kuvunja sheria na akasisitiza kuwa, wale wafugaji wanaodaiwa kulipa fidia baada ya mifugo yao kula mazao ya wakulima, ni lazima walipe.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, aliwataka wakulima na wafugaji kuishi kwa upendo na kuheshimiana ili kupunguza migogoro isiyo na tija.

STORI: ELVAN STAMBULI

Leave A Reply