The House of Favourite Newspapers

Wamepakimbia Bongo

11899492_873726756045040_919698663_nDiamond Platinumz.

LICHA ya muziki wa Bongo Fleva kupiga hatua kubwa hapa nchini, kumekuwa na athari kubwa kwa maprodyuza wa hapa Bongo kutokana na wasanii hao kukimbia kufanya ‘chupa’ zao hapa nchini, badala yake wanakimbilia nje, hasa Afrika Kusini na Nigeria.

Wasanii wengi wanaopenda kufanya video zao nje ya nchi, wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali ikiwemo ubora wa vifaa, kutafuta chaneli za kuonekana kimataifa zaidi pamoja na mazingira mazuri kwa ajili ya video hizo.

Tayari kuna wasanii ambao wameonekana dhahiri shahiri kunogewa kufanya video kwenye nchi hizo na pengine wanaweza kupotea kabisa mikononi mwa ‘Madairekta’ wa Bongo na kuishia kuwasikia tu.

Makala haya yanakuchambulia baadhi ya wasanii ambao kwa hakika inaonyesha ipo kazi kubwa kuwashawishi warudi kutengeneza video hapa nchini kutokana na kauli zao na hata maono yao:

Joh Makini
Anatamba na Wimbo wa Don’t Bother aliomshirikisha staa wa Sauz, AKA ambapo kideo cha wimbo huo kimefanyika katika ardhi hiyo ya Mzee Madiba chini ya Justin Campos na kampuni yake ya Gorilla Films.

Kabla ya kufanya Don’t Bother, Joh pia alifanya video ya Nusunusu nchini humo na kuonekana kutusua vilivyo, hivyo inaonyesha itakuwa kazi kubwa kumrejesha tena Bongo na kufanya kazi hapa nchini kama ilivyokuwa kwa kazi zake za mwisho ku-shoot nyumbani za XO na Bye Bye.

Diamond
Huyu ni miongoni mwa waliokataa kufanya video zake nchini, amelowea Afrika Kusini kwa Godfather ambapo huko amefanyia kideo cha Nana aliomshirikisha Flavour kutoka Nigeria. Kabla ya hapo Mdogomdogo, Ntampata Wapi nazo zilifanyika hukohuko na Number One Remix akaifanyia Nigeria.

Mafanikio anayoendelea kupata kupitia video hizo, si kazi rahisi kumvuta kufanya video nchini kama awali alipofanya za Mbagala, Kamwambie na nyinginezo.

9.1Vanessa Mdee.

Vanessa Mdee
Alianza harakati za kuimba kama masihara alipotoa Wimbo wa Closer chini ya Studio za B Hitz lakini leo anatusua vilivyo katika anga la muziki kimataifa huku Never Ever aliyoachia hivi karibuni ikizidi kumbeba.
Vanessa au Vee Money naye ni mmoja wa wasanii waliopo katika listi ya waliokimbia kutoa video hapa nchini, naye amepata mafanikio zaidi baada ya kuanza kazi na waongozaji wa Afrika Kusini.

4Navy Kenzo
Ni kundi linaloundwa na wasanii wawili, Nahreel na Aika ambao wamekuwa wakitamba na nyimbo mbalimbali lakini kwa sasa wimbo na ubora wa video yao ya Game walioifanyia Sauz ndiyo unawang’arisha hapa nchini na mipaka ya nje ya nchi.
Tayari wameshaonja utamu wa kufanya video nje ya nchi ambapo Game sasa inachezwa katika vituo vikubwa vya hapa Afrika, ikiwemo MTV Base, Sound City, E na stesheni nyingine nyingi maarufu, kwa walipofika ni ngumu kuwarudisha nyumbani kufanya video zao.

Ali Kiba
Tayari ameshafanya video mbili za nyimbo zake nchini Afrika Kusini; Mwana iliyotengenezwa na Godfather na Chekecha Cheketua chini ya dairekta mwenye heshima Afrika, Meji Alabi.

Kutokana na ushindani mkubwa uliopo baina yake na Diamond, inatakiwa kazi ya ziada kumwambia Kiba arejee na kufanya video zake hapa nchini kama ilivyokuwa miaka iliyopita kwenye video za Usiniseme, Cinderela na nyinginezo kwa kuwa tayari ameshaanza kutengeneza njia kubwa zaidi ya kutusua kimataifa.

Wengine
Wengine wanaoonekana kukomaa nchi za nje kutanua ‘carrier’ zao kwa kufanya video kali ingawa si kwa wingi ni pamoja na Linah, A.Y, Ommy Dimpoz, Shettah, Yamoto Band, Madee, Temba na Chegge na wengine wengi wanaozidi kufululiza safari za Sauz na Nigeria kuhangaikia ‘michongo’.

Comments are closed.