The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi HKMU Watia Fora Kwa Tafiti za Afya

0
Profesa Mbembati Naboth, akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Khadija Feruz wa mwaka wa pili udaktari ambaye aliwasilisha mada nzuri kwenye mkongamano la kisayansi.

 

WANAFUNZI  wa udaktari wa Chuo cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), wamepongezwa na kuzawadiwa kutokana na kufanikiwa kufanya tafiti mbalimbali kwenye masuala ya afya.

Tafizi walizofanya zilihusu afya ya mama na mtoto pamoja na magonjwa ya kuambukiza na waliwasilisha tafiti hizo kwenye kongamano la kisayansi lililofanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo.

 

Mkuu wa Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Profesa Mbembati Naboth, ndiye aliwakabidhi wanafunzi vyeti vya kutambua mchango wao wakati akifunga kongamano hilo la siku mbili la kisayansi.

Mkuu wa Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Profesa Mbembati Naboth, akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho waliowasilisha mada nzuri kwenye mkongamano la kisayansi lililofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki. Kushoto ni profesa Columba

 

Profesa Naboth aliwashukuru na kuwapongeza wanafunzi hao kwa kufanikiwa kufanya tafiti nzuri zinazoonyesha hali ilivyo kwenye sekta ya afya huku akiwapa changamoto kuendelea kusoma kwa bidii ili walisaidie taifa kupambana na adui maradhi.

 

Wakati huo huo, wanafunzi hao wameiomba serikali kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa udaktari na uuguzi na kutoa ruzuku kwa vyuo vya afya ili viweze kudahili wanafunzi wengi wa fani hiyo.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Nimrodi Matungwa, alisema ingawa serikali ya awamu ya sita imeonyesha kuwajali lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi wa fani ya uuguzi na udaktari kwani hali ya sasa hairidhishi.

 

“Kwanza tunampongeza sana Rais Samia Suluhusu Hassan kwa mambo mazuri anayoendelea kuyafanya kwenye sekta ya afya ila tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuvipa ruzuku vyuo vya afya vya binafsi ili viweze kudahili wanafunzi wengi wa fani hii,” alisema Nimrodi

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), wakiwa kwenye picha ya pamoja.

 

Alisema iwapo serikali itawekeza zaidi kwenye fani hiyo na kuwapa mikopo wanafunzi wengi wa fani ya udaktari na uuguzi watapatikana wataalamu wengi wa fani hiyo ambao wanahitajika kwenye maeneo mbalimbali nchini kusaidia kutoa huduma za afya.

 

“Hali ya mikopo hairidhishi na takwimu zipo ukiangalia hata hapa kwetu wanaopata mikopo kwaajili ya ada na fedha za kujikimu idadi yetu ni ndogo sana hivyo tunaomba siyo tu kwa vyuo binafsi hata vya serikali wapewe hela ya kutosha ya ada na fedha za kujikimu,” alisema

 

“Kozi zetu ni za muda mrefu sana mfano udaktari ni miaka mitano sasa mtu wa kozi hii akiwa hana mazingira mazuri hasa ya kifedha unamweka kwenye mazingira magumu ya kumaliza masomo yake,” alisema Nimrodi ambaye anasoma udaktari mwaka wa tano.

 

Waziri wa mikopo wa chuo hicho, Elizabeth Mbwambo alisema ni asilimia ndogo sana ya wanafunzi wa fani ya uuguzi na udaktari wanapata mikopo hali ambayo inawafanya waishi kwenye mazingira magumu.

 

Alisema fani ya udaktari na uuguzi zinahitaji vifaa maalum vya kuwawezesha kusoma kwa vitendo hivyo serikali inapaswa kuwasaidia kupata vifaa vyote vinavyohitajika kwenye masomo yao kwa kuongeza kiwango cha mikopo na idadi ya wanafunzi wanaopata.

 

“Ada zetu ni kubwa sasa si wote wanatoka familia zenye uwezo kuna wakati mwanafunzi anafika mwaka wa pili au watatu anapata changamoto ya kuendelea na masomo kutokana na kushindwa kulipa, wakati mwingine analazimika kuahirisha mwaka wake wa masomo kwa kukosa ada,” alisema Elizabeth ambaye anasoma mwaka wa pili uuguzi.

 

Naye Emilia Kitambala aliomba serikali iongeze fungu linalotolewa kwaajili ya tafiti ili kuwahamasisha watafiti vijana kubobea kwenye fani hiyo na hatimaye kuna na majibu ya changamoto nyingi zilizopo hapa nchini.

 

“Serikali iwape kipaumbele kwenye fungu la tafiti na tafiti zikifanyika kuanzia wanafunzi wa shahada ya kwanza ya udaktari zitasaidia sana kutoa ushauri wenye manufaa makubwa sana kwa serikali na tunaomba pia iongeze fedha kwenye masomo ya vitendo,” alisema Emilia ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano udaktari.

 

 

Leave A Reply